Na, Thommy kundy Moshi
Nyakati
za sasa watu wengi wapo bize kuyasaka mafanikio ya kiuchumi kila mahali.
Maisha ya sasa yamekuwa na misukumo na mibinyo mikubwa. Kila kitu kwa
sasa hakiendi ama kufanikiwa pasipo mtu kuwa na uchumi imara, ama kwa
kifupi tuseme fedha.
Fedha
imekuwa ndio "habari ya mjini", inatafutwa kwa udi na uvumba. Suala la
watu kuhangaika na maisha [kutafuta fedha] ni jambo jema; lakini namna
gani (kwa njia gani) watu wanahangaikia hayo maisha ndio jambo
lililoniinua kuandika makala haya.
Nimepata
kufuatilia habari ya Wamarekani tisa marafiki walioshibana ambao
walikuwa matajiri kupindukia lakini utajiri wao waliupata kwa njia za
ujanja-ujanja. Inaelezwa kwamba mwaka 1923 walikutana katika hoteli
maarufu sana ya Hedge-Water; kwa lengo la kuunganisha ukwasi wao ili
wawe na nguvu na sauti zaidi katika uchumi wa taifa lao na dunia kwa
ujumla.(P.T)
Ukwasi
wao [kwa pamoja] ulikuwa ni mkubwa kuliko hazina ya serikali ya Marekani
kwa wakati huo. Walipendwa na kutamaniwa na watu wengi katika mataifa
mbalimbali lakini ilikuwepo siri kubwa sana nyuma ya mafanikio yao.
Licha ya kwamba hawa walikuwa ndio wakopeshaji na wafadhili wakubwa wa
kifedha duniani lakini miisho yao ilikuwa ni mibaya na yenye aibu.
Howard
Hopson alikuwa mmilikiwa kampuni kubwa kabisa ya gesi, iitwayo
Associated Gas and Electric Co. Hadi kufika mwaka 1925 alikuwa na zaidi
ya makampuni 250 yaliyotawanyika kuanzia Ufilipino, Marekani, Kanada na
duniani pote! Mwisho wake ulikuwa ni kufilisika na kufungwa jela baada
ya kufanya udanganyifu kwa wanahisa unaokadiriwa kufikia dola milioni
20.
Charles
Swart alikuwa rais wa kampuni kubwa kuliko zote ya masuala ya chuma.
Mwisho wa huyu bwana ulikuwa ni ufukara baada ya kuishi kwa takribani
miaka mitano kwa madeni. Mwingine ni Samwel Insole aliyekuwa rais wa
kampuni ya kihuduma nae alifariki kifo cha aibu akiwa uhamishoni nchi ya
ugenini. Yupo pia Arthur Carltonn aliyekuwa mfanyabiashara mashuhuri
katika mazao ya ngano nae alifariki akiwa kafilisika yeye na kampuni
yake.
Richard
Whitney yeye alikuwa rais wa soko la hisa la NewYork (NewYork Stock
Exchange). Whitney alijulikana sana kwa maisha ya anasa na alikuja kufia
gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuiba rasilimali za NSE pamoja
na kutoka kwenye benki ya Morgan akishirikiana na kaka yake. Alikuwepo
pia Jesse Luminal aliyemiliki kiwanda kikubwa kabisa cha bia pale Wall
Street baada ya mambo kumuwea magumu aliishia kujinyonga.
Albert
Force nae alikuwa waziri mwenye ushawishi mkubwa sana katika baraza la
mawaziri yeye alifia gerezani kwa kosa la udanganyifu. Lesser Frazer
alikuwa ni rais wa benki ya makazi ya kimataifa nae aliishia kujinyonga.
Ivan Krugar aliyekuwa mmiliki wa kampuni kubwa kabisa nae yalipomfika
shingoni aliamua kujinyonga.
Tupo
katika jamii ambayo inatukuza na kuufurahia fedha zisizo halali; leo hii
mtu anaelipwa laki sita kwa mwezi akiwa hana biashara yeyeote zaidi ya
mshahara wake; ni kawaida kumkuta akiendesha gari la milioni mia moja,
akiishi kwenye nyumba yake binafsi ya milioni mia mbili. Lakini
wanaomzunguka wengi utastaajabia kuona wakimsifu na kumuona kama mjanja
na mtafutaji!
Akili za
wengi sasa zimejikita katika kuvizia fedha za mikato-mikato pasipo
kujali nani anaumia. Watu wanaiba madawa hospitalini watu wanakufa
halafu wakifanikiwa tunasema wamebarikiwa! Watu wakiingia makazini
wanatafuta mipenyo haramu ili kutajirika na "kuyafurahia maisha". Bahati
mbaya ni kwamba hauwezi kuwa na amani [ya ndani] ikiwa mafanikio yako
kifedha yamepatikana kwa njia zisizo halali.
Maandiko
matakatifu yanatuasa kwamba tunapoishi duniani uovu hauwezi kukoma.
Katika uovu huo kuna watu wengi watataka kufanikiwa kwa njia za mikato
mikato na ujanja ujanja; ndio maana tukaambiwa kuwa
usiwahusudu(usiwatamani) waovu(wenye kutumia hila) wanapofanikiwa.
Mtu
anauza unga, mtu anafisadi kazini, anafanya magendo; na sote tunakuwa
tukijua; kisha anajenga maghorofa anamiliki mapesa fedha na utitiri wa
mali; halafu unatamani umfikie? la hasha! Tunaambiwa tusiwatamani kwa
sababu miisho yao ni mibaya. Laana ya kupata mali ama mafanikio kwa hila
haimuachi mtu kirahisi; isipopiga afya yake itapiga familia yake,
isipopiga familia yake itaua jina lake; hayo yasipotokea laana hiyo
itapenya mpaka kwenye vizazi vyake
Leo hii
ukiongea suala la usafi wa kimaadili(hasa katika fedha) watu wengi
watakushangaa. Watakushangaa kwa sababu suala la "kukwapua" limekua la
kawaida sana. Hata hivyo, ukitaka kuwa wa tofauti ni lazima ujizoeze
kufanya mambo ya tofauti. Kama wengine wanaiba, huna sababu ya kuiba kwa
sababu madhara ya wizi, udokozi na ufisadi wako hayatakuwa ya umma bali
ya peke yako wewe mwenyewe.
Wapo
mamia ya wafanyabiashara ambao wanafanikiwa kwa njia ya magendo, kwa
njia ya kuiibia serikali kodi, utapeli na mikato mikato. Watu
wanafurahia mali za kitambo lakini mafanikio yanayopatikana kwa namna
hii mara nyingi huwa hayana mwisho mzuri. Unaweza 'ku-win' wewe lakini
ukakiachia kizazi chako matatizo makubwa usivyodhania.
Ni vema
kujifunza kutafuta mafanikio na utajiri wa haki. Kwa mujibu wa maandiko
matakatifu[Biblia], utajiri na mafanikio ya haki yana sifa kubwa tatu.
Kwanza yanakuwa ya kizazi na kizazi, pili hayaambatani na majuto na tatu
yana ulinzi wa kuaminika. Vile vile maandiko yanatutahadharisha kwamba
mafanikio na utajiri vilivyopatikana kwa pupa hutoweka ghafla
Kuna
umaana gani mtu kuwa na mali leo halafu watoto wako wakaishia kuwa
ombaomba ama vizazi vyako vikakosa cha kurithi na kukukumbuka? Kuna haja
gani mtu kuwa na utajiri mkubwa halafu uishie kuwa na mikasa
itakayokuletea majuto? Fikiria mfanyabiashara anaefanya biashara kwa
kukwepa kodi, siku akikumbana na mkono wa dola akafalisiwa bila shaka
ataishia kwenye majuto makubwa.
Watu
wanapata mafanikio na utajiri kwa njia ambazo zinahatarisha hadi afya
zao (misongo, mawazo, misukosuko); mwisho wanajikuta wakipata presha,
magonjwa ya moyo na madhara mengine yatokanayo na kukosekana msawazo wa
kimwili. Sasa kuna haja gani ya kuwa na mafanikio na mali ambavyo mwisho
wa siku vitakuja kutumika kugharimia kutibu afya yako?
Utajiri
na mali zinazopatikana kwa hila ama ujanjaujanja hazidumu, hazina uhuru
nakamwe hazina heshima pia.Namna zlivyopatikana ni siri ya mhusika.Mtu
mwenye mafanikio ya jinsi hii hayuko huru hawezi kueleza kwa uwazi
chimbuko la utajiri wake.Na ikilazimu basi kufanya hivyo atasema uongo
tu!Kweli utawadanganya wengine lakini dhamira yako ya ndani haitaacha
kukusuta,hamna heshima hapo!
Wanasema
pesa inaleta heshima, pesa sabuni ya roho; hata hivyohilo linategemeana
umezipataje.Hebu fikiria mtu anayepata pesa na mali kwa njia ya utapeli,
dhuluma kwa wanyonge,kuudhalilisha mwili wake,kukatisha maisha ya watu
wasio na hatia kwa kumwaga damu zao ili mradi tu ufanikiwe; Je hiyo ndio
heshima yenyewe? Ama sabuni gani inayotokana na ubaya wa namna hii?
No comments:
Post a Comment