Blogger Widgets FURSA KWA VIJANA WOTE TUPAMBANE KWA KILA NJIA ILI MRADI TUWEZE KUEPUKA HUU UMASKINI TANZANI NA AMIN KILA ATAFUTAYE KWA NIA HUPATA MAANA ATA MAANDIKO HUSEMA PENYE NIA PANA NJIA

Tuesday, October 14, 2014

Asasi za Vijana na Taifa Tulitakalo!

Asasi  za  vijana ni makundi ya vijana  yaliyosajiliwa na serikali kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za umma kwa maendeleo ya nchi na vijana wenyewe kwa ujumla.
Asasi za vijana nchini Tanzania kwa mujibu wa Wizara ya Vijana, Habari, Utamaduni na Michezo kupitia Sera ya Vijana ya Taifa ya mwaka 2007 zimeshafikia zaidi ya 6000.  Asilimia kubwa ya asasi hizi  zimeundwa na vijana, huongozwa na vijana katika kutetea masuala mbalimbali ya vijana nchini. Miongoni mwa asasi hizi za vijana ni kama; Tanzania Youth Vision Association (TYVA), Youth for Africa (YOA) na United Nations’ Clubs.
Kulingana na majukumu yake na lengo la kufikia vijana wengi popote walipo nchini Tanzania, asasi hizi zimesambaa mikoa mbalimbali kama vile jijini Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mbeya na miji mingine nchini.
Vijana wanaoshiriki katika asasi hizi baadhi huitwa “vijana wanaharakati” kutokana na kuongea na kuonekana wakitetea masuala mazito ya makundi yaliyopo pembezoni na kwa nyakati nyingine kupigia chapuo ubadilishwaji wa sera mbalimbali. Baadhi ya vijana wanaharakati wameshapitia nyakati ngumu katika shughuli zao hizo za kusimamia maslahi hususani ya wanyonge jambo ambalo limepelekea baadhi kutishiwa au hata kukamatwa. Lakini  yote ni katika kuleta ustawi wa vijana na makundi mengine katika jamii yetu.
Vijana wengi kwenye hizo asasi wamejitahidi kujadili, kufanya uchunguzi na  kutafuta suluhu ya changamoto zinazolikabili Taifa mathalani ukosefu wa ajira,  njaa, umasikini, magonjwa , na fursa duni za kupata teknolojia ya kisasa na kwa bei nafuu..
Mtazamo wa Jamii
Kuna mtazamo ambao wanajamii mbalimbali wanaotuzunguka wanao juu ya asasi za vijana. Wanajamii wanadhani kwamba kushiriki katika harakati hizo ni uhuni au upotezaji wa muda. Lakini ukweli si huo kwani kwa kujihusisha kwenye mambo mbalimbali na watu wa rika yako inasaidia sana na kuongeza upeo wa kufikiri na kuchukua maamuzi sahihi maishani.
Hivyo basi uwezo wa akili unapanuka zaidi na kufikiri mambo ya maendeleo zaidi kuliko kuwa na ufinyu wa akili, kuwaza mambo maovu yenye kujaa uzembe na kubweteka, kuingia kwenye makundi yasiyo na mbele wala nyuma katika maisha yako ya sasa na baadaye.
Ongea na Watu, Uvae Viatu!
Kwenye hizo asasi vijana wanajifunza mengi yanayohusu ujana wao na maendeleo kwa ujumla. Waswahili husema; “Ongea na watu uvae viatu” kwa msingi huo utajua mengi sana ukiwa katika makundi ya wanaharakati vijana.  Hii ni dhahiri kwani vijana ni taifa la leo na kutafuta maendeleo ni lazima ili kutengeneza jamii yenye mwamko wa mabadiliko chanya. Kiukweli kuna vijana waliokuwa wakijituma huko nyuma na wengine wanaendelea kujituma sana kwenye hizi asasi za vijana nchini na maendeleo yao yanaonekana kwenye jamii zetu kwa kuwa wamekuwa mfano bora wa kuigwa katika ngazi walizopo.
Asasi Zimetoa Viongozi!
Baadhi ya asaasi na taasisi hizi za vijana tayari mchango wake umeanza kujidhihirisha katika jamii. Kuna  vijana ambao walipitia na kuwa viongozi katika asasi hizi na sasa wameweza kushika nyadhifa mbalimbali za kiuongozi katika tasnia mbalimbali nchini mathalani katika siasa, serikalini, mashirika ya umma na yale ya binafsi.
Tunawaona leo wabunge vijana tena machachari kama Zitto Kabwe, John Mnyika , David Kafulila, Halima Mdee na wengine wengi. Uchapakazi na utendaji kazi wao umekuwa mrejesho chanya kwa mchango wa taasisi zile za vijana walizopita na pia umuhimu wa kuwapo kwa taasisi imara za vijana nchini.
Lakini licha ya viongozi hao wa kisiasa, wapo viongozi wengine wengi vijana katika sekta binafsi mathalani mjasiliamali Paul Mashauri ambaye naye ameshiriki kwa kiasi kikubwa katika taasisi mbalimbali za vijana.
Tukiangalia pia upande mwingine wa shilingi, kuna vijana kama Togolani Mavura toka Wizara ya Mambo ya Nje na kundi jingine kubwa ambalo limo serikalini katika ngazi mbalimbali ambao katika ujana wao wamekuwa sehemu ya mashirika mbalimbali ya vijana na kuweza kupanua wigo wa kifikra na mtizamo katika masuala mbalimbali.
Taifa likiwa limeingia katika mchakato wa kupata katiba mpya, tunaona sura ya uwakilishi wa kijana, Humphrey Polepole katikati ya kundi la wataalamu wa fani kadha wa kadha akiwakilisha maslahi ya nchi na kwa kiasi fulani pia uwakilishi wa ujana katika Tume ya kuratibu Mchakato wa Katiba Mpya. Yeye akiwa ni zao la mashirika ya kiraia ya vijana nchini Tanzania.
Mifano ipo mingi na dhahiri, kwa majina na wale ambao wameshiriki kwa nafasi mbalimbali  hata kama makala hii haiwezi kuwataja wote, lakini kuwa kwao katika ujenzi wa Taifa letu kupitia nyanja mbalimbali wanaonyesha ushiriki wao katika mashirika haya ya vijana halikuwa jambo la bure wala la kupoteza muda. Bali imekuwa ni tunu idumuyo daima katika mhusika kufuatana na kiwango cha ushiriki wake na ari ya kujifunza na kutenda.
Hawa daima wanatoa funzo kuwa taasisi hizi za vijana zinaitaji kuimarishwa, kutoa wigo wa utendaji kazi zake na pia kuhamasisha vijana wengine wengi zaidi na zaidi kushiriki.
Kwa Wazazi na Jamii Yote!
Wazazi na jamii kwa ujumla wanatakiwa kuwa na mtazamo chanya na kuacha fikra potofu juu ya asasi hizi za vijana nchini. Kwani dunia ya sasa ni ya kujua mengi na kujituma. Bila hivyo ni sawa na kutembea gizani bila kujua mbele kuna nini.
Kuna wazazi wengine wanawazuia vijana wao kushiriki kwenye shughuli za kijamii zikiwemo za asasi za vijana wakidhani vijana hao wanapotea lakini wajue kila kitu kinaenda na mabadiliko na hii ni sehemu ya mabadiliko.
Shukrani kwa wabia wa Maendeleo mbalimbali ambao wapo mstari wa mbele kusaidia na kushirikiana na mashirika ya vijana kwa hali na mali. Mchango wao usiokoma ndiyo unaoimarisha sana uwepo wa mashirika haya.
Kwa upande mwingine pia, Serikali hususan kupitia Wizara ya Vijana, Habari na Utamaduni bado wanajukumu kubwa la kuhakikisha mashirika haya yanasimama imara na kuzidi kutoa mchango wake kwa vijana wengi zaidi kwa maslahi ya ukuaji bora wa vijana na Taifa kwa ujumla.
Kijana Amka Ushiriki!
Kesho haitafika bila ya jana. Maendeleo hayaji bila kujituma na kupanua uwezo wa kufikiri. Ni vizuri kwa kijana yeyote ashiriki ipasavyo katika shirika la vijana ambalo anapenda hasa akiongozwa na malengo na kazi za shirika husika. Kwani; “Mkaa bure, si sawa na mtembea bure”! Kwa kushiriki katika mashirika hayo, ndipo kijana atamudu kuongeza mtandao wake wa kufahamiana na vijana wenzake wengine wenye uwezo na maarifa mbalimbali ambayo kutoka kwao ataweza kujifunza zaidi na zaidi na hatimaye kujipatia maarifa adhimu kwa ustawi wa maisha yake kwa wakati huu na hata baadae.

No comments:

Post a Comment

TUPAMBANE BLOG