Blogger Widgets FURSA KWA VIJANA WOTE TUPAMBANE KWA KILA NJIA ILI MRADI TUWEZE KUEPUKA HUU UMASKINI TANZANI NA AMIN KILA ATAFUTAYE KWA NIA HUPATA MAANA ATA MAANDIKO HUSEMA PENYE NIA PANA NJIA

Thursday, October 16, 2014

: Kilimo ni Msingi wa Changamoto za Ajira kwa Vijana wa Liberia



Na Travis Lupick


Akiwa na mkufu wa dhahabu, kofia na kuvalia kamptula fupi, Junior Toe alikuwa amevaa nguo zinazovaliwa na vijana wa mjini nchini Liberia. Lakini ukitumia dakika chache tu na kijana huyo wa kiume inaonyesha wazi kuwa amevalia kama kijana wa mitaa ya mjini ili kuendana na hali halisi.

MONROVIA, Julai 31 (IPS) -
Hata hivyo, sehemu ya maisha ya Toe inaonekana kuwa nje ya jiji na iko shambani.

"Angalia mbegu za pilipili pale," anasema wakati akitembelea shamba la jumuiya ambalo haliko mbali na mjini Monrovia. "Ziingize kwenye udongo, zimwagilie maji mara chache, utaweza kutengeneza pesa."

Toe ni mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Mtandao wa Vijana katika Jamii (CYNP), ambao unatoa mafunzo kwa vijana kuhusu kilimo na ufugaji wa mifugo.

"Pale tuna kitalu cha kabichi, ," anaendelea. "Kama unajaribu na kupanda kabichi katika udongo sasa, mvua zitaiathiri vibaya. Haya ni aina ya maarifa ambayo tunabadilishana."

Usalama wa chakula na ajira kwa vijana wa Liberia kwa muda mrefu vimekuwa ni changamoto katika taifa hili la Afrika Magharibi. Kwa sasa, idadi kubwa ya mipango inayojikita katika jamii na mipango ya serikali inafanya kazi kushughulikia matatizo haya mawili. Viongozi wa serikali wanasema wana matumaini kuwa huu ni mwanzo wa kubadilika kwa vijana wa Liberia juu ya jinsi ya kushiriki katika sekta ya kilimo.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2010 ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, asilimia 30 ya ardhi nchini Liberia inafaa kwa kilimo na karibu asilimia 90 ya maeneo yenye mazao yanapata mvua za kutosha. Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Usalama wa Chakula Liberia ya mwaka 2012, asilimia 60 ya wakazi wako katika kundi la "watu wasiokuwa na usalama wa chakula".

Sekta ya kilimo nchini Liberia iliharibiwa vibaya wakati wa miongo ya kukosekana kwa usimamiaji na vita. Mwaka 1980, Sajenti Samuel Doe alichukua madaraka katika mapinduzi ya kijeshi na utawala wake, ambao ulidumu kwa miaka 10 baadaye, ulikuwa na sifa ya kuwepo kwa sera mbovu ambazo zilikuwa kikwazo kwa maendeleo.

Mwaka 1989, nchi iliingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilidumu hadi mwaka 2003. Katika miaka yote hiyo ilishuhudiwa mbabe wa kivita – na baadae kuwa rais– Charles Taylor akipora rasilimali za nchi na kusababisha ghasia zilizowaua watu 250,000. Idadi kubwa walikimbia kutoka Liberia.

Kwa mujibu wa tathmini ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), ya mwaka 2009 kati ya mwaka 1987 na 2005 uzalishaji wa chakula kama vile mpunga, ulishuka kwa asilimia 76.

"Uzalishaji wa kilimo uliongezeka katika miaka ya karibuni wakati sekta ikifufuka polepole, lakini mavuno bado yapo chini ya wastani wa kikanda na kukosekana kwa usalama wa chakula kuko juu mno,"inasema ripoti hiyo ikiongeza kuwa Liberia bado inazalisha tu kiasi cha asilimia 40 ya mpunga unaohitajika kulisha wakazi wake wapatao milioni nne.

Pia walioathirika na vita ni vijana wa Liberia, ambapo makumi kwa maelfu kati yao walilazimishwa kujiunga na vikundi vya waasi wakiwa ni wavulana na wasichana wa umri mdogo. Miradi ya kuwajenga upya iliyoendeshwa na Umoja wa Mataifa ilijaribu kuwaunganisha tena wapiganaji wa zamani na waathirika wa vita, lakini programu hizi sasa zinakosolewa mno kuwa zimeshindwa.

"Nilipitia mchakato wa kupokonywa silaha, katika mafunzo ya wiki moja," Toe anasema, huku akionyesha uso wa dharau.

"Lakini watu wengi hawakuona kuna faida kufanya hivyo ….Watu waliathirika kisaikolojia; walikuwa wamezoe bunduki, walikuwa wamezoea kuwa na pesa, na walikuwa wamezoea kupata mara moja kile walichokitaka"

Toe anasema baada ya kuona madhaifu ya programu za kuwajenga vijana, aliamua kuanzisha programu yake mwenyewe, ambayo ingefaa kwa Liberia. Alitoa sababu kuwa kwa kuwa na ardhi yenye rutuba na hali ya hewa ya joto na ya mvua, kilimo kilikuwa ni njia ya kufuata. Hivyo alianzisha CYNP mwaka 2007.

Shirika hilo sasa lina kituo cha kutoa mafunzo cha Bensonville, Kata ya Montserrado (kama saa moja kwa gari kaskazini mashariki mwa Monrovia). Katika kata hiyo, ardhi imegawanyika katika mashamba nane ambapo wanafunzi wa zamani na washirika wao wanaendesha vipande vya mashamba iwe wao wenyewe au katika ardhi ya jumuiya. Jukwaa la Wakulima Vijana linawafanya washiriki kuunganishwa na kufanya kazi kujenga uelewa na kuvutia wakulima wapya.

Jambo muhimu kwa mafanikio ya CYNP, na kinachoifanya kuwa tofauti na kazi ya zamani ya Umoja wa Mataifa kwa wapiganaji wa zamani, ni kusisitiza katika umiliki. "Tunafanya kazi na nyie kuendeleza miradi yenu wenyewe katika jamuiya yenu," Toe anasema.

Kwa mujibu wa Toe, kwa sasa kuna vijana wapatao 100 ambao wamejiunga katika programu ya miezi sita katika eneo la Bensonville, na wahitimu wapatao 500 kwa sasa wanaendesha kilimo katika jumuiya zao kuzunguka Montserrado.

Idadi kadhaa ya wahitimu wanaweza kupatikana wakifanya kazi katika vipande vyao vya ardhi katika ardhi ya serikali isiyotumika katika kitongoji cha Fiamah mjini Monrovia. Alfred Kapehe anasema kuwa CYNP ilimsaidia kuendelea kutoka mkulima mdogo wa kujikimu hadi mkulima mdogo wa kilimo cha biashara. Vile vile, James Paylay anasema shamba dogo analolima linamletea fedha za kutosha kuweza kukodisha nyumba kwa ajili ya familia yake, na kulipia watoto wake ada ya shule.

"Kila kitu kinatokana na bustani," Paylay anasema.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Vijana wa Liberia Sam Hare anakubali na kutaja mara kwa mara takwimu za USAID zikionyesha kuwa asilimia tatu tu ya vijana wa Liberia wanavutiwa na kilimo. Lakini, katika mahojiano na IPS, anasema kuwa hali hiyo inabadilika.

"Kilimo kimebainishwa kama suala la msingi katika kuondokana na changamto ya ajira kwa vijana," anasema.

"Tumefanya kazi na Wizara ya Kilimo na wadau wengine kuwafanya watu kuona kuwa kilimo, kikiangaliwa kwa mtazamo sahihi, ni chombo cha utajiri."

Hare anasema kuwa changamoto ni kushawishi vijana kuwa wanaweza kufanya kazi shambani kuvuka kilimo cha kujikimu na kuwa wakulima wa biashara.

"Vyuo vyetu vya ufundi stadi sasa vinapaswa kuwa na maana tofauti na kupangwa upya ili kukidhi mahitaji ya Liberia. Na vijana na kilimo iwe jambo la kipaumbele," anaongeza.

Joseph Boiwu, ofisa mipango wa FAO nchini Liberia, anasema kuwa kikwazo kingine kinachowafanya vijana kushindwa kuingia kwenye kilimo ni kutokana na kazi yenyewe kuhitaji nguvukazi kubwa. Kutafutia ufumbuzi wa tatizo hili FAO na washirika wengine walisambaza matreka 24 ya power tiller kwa vikundi vidogo vya wakulima katika kata za Bong, Lofa, na Nimba mwaka 2010.

"Kwa sasa tutakwenda kufanya upya tathmini kujua dhamira ya vijana kujiunga na kilimo," anasema Boiwu. Kama mpango huo utafanikiwa, utaweza kukua na kuhusisha mashine kubwa kama vile matrekta.

Prince Sampson, mkuu wa Chama cha Maendeleo ya Vijana kaskazini ya kati mwa Liberia, anaelezea mpango wa shirika lake kuendesha shughuli sawa na CYNP. Kama ilivyo kwa Toe, anasema kuwa alijifunza kutokana na makosa wakati wa warsha baada ya vita ambazo zilishindwa kuwekeza vitega uchumi vya muda mrefu kwa watu.

"Wapiganaji wa zamani walikuwa na mafunzo ya ufundi seremala, kujenga nyumba, na maarifa mengine," Sampson anasema.

"Na halafu baada ya hapo hakukuwa na kitu chochote chenye tija kukifanya. Una watu waliopatiwa mafunzo, halafu hawakuwa na chanzo cha kipato. Walirejea chini kabisa."

Sampson, ambaye amekuwa akifanya kazi na vijana walioathirika na vita tangu mwaka 1992, anaendelea kusema kuwa kilimo ni tofauti kwasababu kina uwajibikaji wa karibu.

"Vijana wanakula mpunga walioupanda. Mboga mboga zinauzwa, faida zinagawanywa miongoni mwao na wanakuwa na pesa mifukoni."

Sampson anaelezea umuhimu wa kushirikisha wapiganaji wa zamani nchini humo katika kilimo kama suala la usalama wa chakula.

"Tunawafanya kuelewa faida ya miaka ambayo bado inakuja mbeleni mwao, pamoja na miaka mingi ambayo waliipoteza wakiwa vitani ," anasema.

"Tunawafanya kuelewa kuwa nguvu walizonazo – moyo wao wa ujana bado unaweza kutumika kwa mafanikio."

*Taarifa za nyongeza kutoka kwa Al-Varney Rogers mjini Monrovia. (END/2012)




No comments:

Post a Comment

TUPAMBANE BLOG