Na Pr.Thommy kundy Moshi
Kazi ya uchungaji ni
kazi nyeti tena ya muhimu sana katika jamii yoyote. Unapoitwa mchungaji
umebeba jina ambalo ni la heshima kupita Rais wa nchi. Hivyo jamii
yoyote unapotamka kuwa wewe ni mchungaji wanaanza kupiga picha mtu
ambaye ni mtakatifu asiyeweza kukutwa na tuhuma yeyote na pia
asiyekosea. Hivyo ijapokuwa ni dhana iliyojengeka kwa jamii bado
yatupasa kuiheshimu dhana hiyo kwa kuzingatia miiko ya kichungaji. Yapo
mambo ya msingi wewe kama mchungaji unapaswa kuzingatia.
Miongozo yetu ya kanisa [Church Policy,
Church manual, Ministers Manual, Pastoral Ministry, Elder’s Handbook,
n.k.] imeweka wazi mambo ya msingi ambayo yanaweza kukuongoza (kukupa
‘Guideliness’) nini cha kufanya au usifanye (Dos and Don’ts).
1. Mchungaji
unapaswa utambue kuwa umeitwa katika utumishi na wala sio ajira (It is a
call but not a career) hivyo hutazamiwa kukutwa kwenye mgomo wowote kwa
mambo ambayo hukubaliana nayo kama vile mshahara hautoshi, kugomea
maagizo ya uongozi, au kuendesha migomo kwa washiriki dhidi ya uongozi
wa ngazi za juu kwa jambo lolote ambalo hujaliafiki. Maana ya “wito ni
kwa kawaida unaanza kwa shauku ya kujali hali ya kiroho ya wengine na
kuhubiri neno la Mungu"
2.
Mchungaji unapaswa kutambua kuwa umeitwa kwa ajili ya injili na wala
sio kwa ajili ya cheo au kitu chochote. Hivyo hupaswi kutazamia swala la
kupanda cheo au kufanya kampeni kwa ajili ya kupanda cheo.
3.
Mchungaji hupaswi kuwa na tuhuma yoyote ambayo italeta aibu kwa kanisa
au taaluma yako. Tuhuma hizi ni pamoja na Uasherati, Uzinzi, wizi wa
fedha, n.k.
4.
Epuka kutembelea washiriki walio wa jinsia tofauti na wewe nyakati za
usiku au mahali ambapo hakuna watu mkiwa peke yenu. Usijaribu kutembelea
wajane, wasichana, au waliotelekezwa peke yake bila mzee wa kanisa au
shemasi mkuu wa kiume au mke wako.
5.
Mchungaji epuka madeni kama ukoma kutoka kwa washiriki au watu ambao
sio waumini au mashirika yoyote. Rafiki wako wa karibu unapokuwa na
shida ni ofisi yako ya Konferensi au mtendakazi mwenzako. Bali uwe
mwaminifu kulipa kwa wakati.
6.
Mchungaji unapaswa kutokuwa na makundi ndani ya kanisa au kwa
watendakazi wenzako. Hili linamaanisha hupaswi kuligawa kanisa katika
makundi yoyote. Jaribu kufanya kila linavyowezekana kuleta umoja hata
kwa wale ambao hawapendi umoja au wasiokuafika kwa kazi yako na uongozi
wako.
7. Mchungaji
unapaswa kuwa mwalimu au muhubiri. Kinachotazamiwa kwa mchungaji ni
kuwa mfundishaji zaidi kuliko kuwa mhubiri kwa ajili ya kuelimisha
kanisa. “Usijaribu kuwa muhubiri bali uwe mtendakazi wa Mungu.”
8.
Mchungaji unapaswa kuunga mkono programu zote za kanisa bila kuwa
kinyume na program hizo. Epuka kupinga kwa njia yoyote mipango kutoka
juu au jambo jipya ambalo hujalielewa. Fundisha mafundisho yote ya
kanisa na kanuni zake.
9.
Sukuma idara zote ndani ya kanisa bila kupendelea idara yoyote. Hili
likiwa na maana kupenda idara zote kwa kuzihamasisha bila kuwakatisha
tamaa viongozi wake makanisani.
10.
Mchungaji unapaswa kuhudhuria mikutano ya kanisa kama vile maombi ya
jumatano, kufungua sabato, na kufunga sabato, makambi, efoti, unapokuwa
karibu na matukio hayo yote.
11.
Mchungaji unapaswa kuheshimu kazi ya mchungaji mwenzako uliyempokea
mtaa au ofisi. Usikubali kujadili madhaifu ya mchungaji mwenzako
uliyempokea kwani kufanya hivyo unaharibu heshima ya kazi ya kichungaji.
Epuka kudharau mipango yake aliyoacha bali unapaswa kuisapoti mipango
yake mizuri kisha ingiza yako taratibu kwa hakika bila kukashifu yake
unayoiona kuwa ni mibovu.
12.
Mchungaji unapaswa kusimamia mabaraza yote ya uchaguzi kwa ajili ya
kuchagua viongozi watakaokusaidia kazi yako kwa mwaka huo. Ni jambo la
lazima na la muhimu labda itokee tu kuwa wewe ni mgonjwa ama unadharura
ya muhimu sana. Lakini ni vizuri kuteua mtu anayeweza kuwakilisha
vizuri ndani ya baraza hilo ama uruhusu wachague mwakilishi lakini uwe
umejulishwa pendekezo hilo.
13.
Mchungaji uwe kielelezo nyumbani kwako kwa kuwa na ibada ya asubuhi na
jioni kwa familia yako. Nunua lesoni za watu wazima, na za watoto ikiwa
wapo wadogo.
14.
Mchungaji unapaswa kuwa wakili mwaminifu kwa kutoa zaka na sadaka,
kuwahi kwenye vikao vya kanisa au matukio yoyote, na pia kuwahi ibada
kanisani. Epuka kutoa muda wa kukutana bila kufika kwa wakati mliopanga
pamoja au uliotamka watu kuhudhuria kama vile mabaraza ya kanisa,
semina, na kazi za mikono za kanisa.
15.
Epuka sana kutumia fedha za zaka na sadaka ya konferensi (‘trust fund’)
bila idhini ya ofisi. Usijaribu kukopa kwa njia iwayo yote au
kuendeshea miradi yako kwa madhumuni ya kurudisha baadaye.
16.
Usichukue fedha ya kanisa kwa matumizi yoyote bila idhini ya kanisa
lote yaani mashauri ya kanisa. Usiende kwa mhazini wa kanisa kuchukua
fedha yoyote bila uongozi wa kanisa kujua au kukupatia. Fanya kazi yote
kupitia kwa mzee wa kanisa.
17.
Mchungaji unapaswa kupeleka taarifa kila mwezi na taarifa za robo kwa
wakati ili kutoa taarifa kwa uongozi wa juu swala la utendaji wako wa
kazi katika mahali unapofanya.
18.
Mchungaji unapaswa kuepuka ukabila au ubaguzi wa jinsia au hadhi
(wasomi na wasiosoma au matajiri na maskini au mlemavu na asiye
mlemavu).
19.
Mchungaji unapaswa kufurahia maisha uliyonayo na pia ishi maisha ya
kawaida bila hofu. Usitake kufanana na wengine wakati uwezo huna
utaingia katika madeni na chuki.
20.
Mchungaji unapaswa uwe mwaminifu kwa watu na kwa Mungu. Hasa unapopewa
fedha na ofisi jitahidi kutoa taarifa ya kweli kwa matumizi uliyofanya.
Kumbuka jicho la Mungu linaona kila wazo na kila tendo.
21.
Mchungaji epuka kile kinachoitwa ‘conflict of Interest’. Kitu
kinachofuja muda wako wa kazi au kinachopingana au kushindana na huduma
ya kichungaji kama vile biashara za masafa marefu, hospitali, duka la
dawa, mradi wowote mahali ambapo kanisa nalo limeweka yake, uendeshaji
wa miradi mikubwa kama vile shule, zahanati, viwanda, n.k.
22.
Mchungaji hupaswi kujiunga na vikundi vya siri (secret society) ambavyo
vipo ulimwengu katika kuendesha mipango ambayo ni ya uhalifu, na
biashara mbaya. Pia kujihusisha na uchezaji wa michezo ya bahati nasibu
kwa ajili ya kujinufaisha kimaisha au kimapato. Hii inamaanisha tuache
kucheza michezo yote inayotupatia mapato ya aibu. Soma kitabu cha
Mashauri Juu ya Uwakili.
23.
Mchungaji unapaswa kuonyesha mfano mzuri kwa familia yako kwa kumfanya
mwenzi wako kuwa msiri wako na tena mfariji wako. Hivyo magomvi na
mahusiano mabaya dhidi ya mwenzi wako ni sumu ya kazi yako uchungaji.
24.
Mchungaji unapaswa kuishi kwa kushabihiana na kile unachofundisha
kulingana na msingi wa mafundisho ya imani yetu ya kanisa la
Waadventista Wasabato. Epuka kutoa mafundisho mapya ambayo kanisa
mahalia wanakuwa na mashaka nalo bila kutafuta msaada kutoka kwa ndugu
walio watendakazi wenzako ili kujua msimamo wake.
25.
Mchungaji unapaswa kila wakati kutafuta kupanda mafanikio. Unapaswa
kutafuta kiwango cha juu katika kazi yako. Hii ndio siri ya mafanikio
katika huduma yako.
26.
Mchungaji hupaswi kujiamini mwenyewe kupita kiasi; kwani jambo hili
limesababisha wengi kuwa na dharau kwa watendakazi wenzao, na tena
kushindwa kushaurika mahali anapokosea.
27. Mchungaji
unapaswa kumheshimu mchungaji uliyepewa kama msimamizi wa kazi
anayekufundisha kazi (Intern Supervisor). Furahia mashauri yake ili
uweze kufaidi uzoefu wake. Mama White anasema, “Hebu Watendakazi wa muda
mrefu (older workers) wawe waelimishaji, wajitunze wenyewe chini ya
nidhamu ya Mungu. Hebu vijana wajisikie ni fursa (privilege) kujifunza
chini ya watendakazi wa muda mrefu, na hebu wao wabebe kila mzigo ambao
vijana na uzoefu wao vitaruhusu. Kama vile Eliya alivyowaelimisha vijana
wa Israeli katika shule ya manabii;vijana leo wanahitaji kuwa na
mafunzo kama hayo hayo. Haiwezekani kushauri kwa kila kipengele katika
sehemu ambayo vijana wanapaswa kutenda; lakini wanapaswa kuelekezwa
uaminifu na watendakazi wa muda mrefu (older workers), na kuwafundisha
kumtazama daima Yeye (Yesu) ambaye ni mwenye kuanzisha na kuitimiza
imani yetu.”
“Kipindi
chote cha ajira kabla mtendakazi mpya (anayeanza kazi) hajawekewa
mikono anapaswa inapaswa afikiriwe sana sehemu ya mafunzo yake. Miaka
yake miwili ya kwanza, hususani, inapaswa isimamiwe kwa ukaribu zaidi.
Msimamizi anapaswa kufikiriwa mtu anayefaa (au mwenye sifa) ya kusimamia
asimamie tu mara baada ya kuchukua mafunzo maalumu kama haya
yanayotolewa na kozi hii.”
SIRI YA MAFANIKIO KWA MCHUNGAJI UNAPOONGOZA MTAA MKUBWA.
Kanisa la
Waadventista Wasabato katika Afrika, Asia, Amerika ya Kusini, n.k
wachungaji wake wengi wanaongoza makanisa mengi kutokana na uhaba wa
watendakazi na pia hali ya uwezo wa kuajiri au kusomesha watendakazi
wapya. Hivyo inalazimu mchungaji kuchunga au kuongoza makanisa kuanzia
matatu hadi ishirini na mbili. Jambo ambalo halileti ufanisi kwa
mchungaji kuweza kutekeleza majukumu yako kama mchungaji kama vile
kuwalisha kiroho, kuwatembelea mshiriki mmoja na kuomba naye, kuendesha
huduma za meza ya Bwana, n.k. Hivyo ili kufanikiwa wewe kama mchungaji
wa mtaa ya mambo yatakayokusaidia. Nayo kama ifuatavyo:-
1. Wafundishe
wazee wa kanisa huduma ya kichungaji (uongozi wa huduma ya kichungaji)
na kuwatengeneza wafae kwa uongozi wa kanisa. Wafanye wawe na mzigo wa
kulea washiriki, kuhubiri, kufanya uinjilisti, kutoa elimu ya Kikristo,
na kutunza mali za kanisa.
2.
Ujihusishe katika kila aina ya makusanyiko ya washiriki. Hili linahusu
kuwa na ratiba ya ziara zako na mambo yako (itinerary). Unapofika katika
kanisa lolote la mtaa wako hakikisha unahudumu siku hiyo maana wazee wa
kanisa na washiriki wamekuwa na muda mrefu wa kuhudumiana wakati haupo.
Pia mchungaji uwe na ratiba ya dharura panatokea misiba, kuwaona
washiriki walio wagonjwa taabani. Ndoa na ubatizo hakikisha unatoa
msisitizo wa huduma hizi zipangwe vyema.
3.
Toa mafunzo ya ujuzi wa kichungaji kwa viongozi wa kanisa kama vile
wazee wa kanisa na mashemasi. Fanya hili kwa vitendo kwa Kuendesha
mikutano ya kamati mbalimbali, Namna ya kuandaa hubiri na kulihubiri;
utembeleaji wa washiriki wenye ufanisi; Imarisha idara za kanisa; Namna
ya utunzaji wa mali za kanisa; Fundisha kwa kina kuuelewa ujumbe wa
Kiadventista; na namna ya utunzaji wa waumini wapya.
A. Mwaka
1991 General Conference kikao chake cha mwaka kilipendekeza kuwa
“Fildi/Konferensi kuendesha kwa kiwango cha chini Semina moja ya Mafunzo
kwa Wachungaji na wazee wa Kanisa kila Mwaka. Ikiwa ni muhimu, makanisa
yanapaswa kulipia gharama za usafiri kwa wazee wao kwa kuhudhuria
semina hii.”
B. Wachungaji
wa Mitaa vile vile wanapaswa kupanga na wazee wote katika mtaa wake
kila mwezi au kwa miezi miwili. [Nyongeza yangu: kuwa na kikao cha
kupanga kazi yaani baraza la mtaa kutoa semina na mipango ya mtaa wako].
Mikutano hii italenga kupanga mipango kwa mtaa na makanisa. Mipango hii
itashughulika na uinjilisti, kufungua maeneo mapya katika mtaa, masomo
ya kuhubiri, utembeleaji, magoli ya makanisa na mtaa, ratiba (itenerary)
ya mchungaji na mipango yake.
4.
Toa hamasa kwa kanisa kuendesha mahubiri na ubatizo wa mara kwa mara.
Na pia hamasisha makanisa kuona umuhimu wa kuendesha meza ya Bwana kila
robo na pia utoaji wa taarifa kila robo. Toa umuhimu wa makanisa kuwa
mikutano ya mashauri kila mara kwa kadiri iwezekanavyo ili kuleta umoja
na uwazi kwa mipango ya kanisa.
MAMBO YA FEDHA YA KUZINGATIA.
1.
Mchungaji unapaswa kutambua kuwa wewe ni mkaguzi namba moja wa kanisa
na pia kumfundisha mzee wa kanisa namna ya kukusaidia kukagua fedha za
kanisa. Hakikisha uwe na wivu na mali ya Bwana yaani mlinzi wa hazina ya
Mungu. Pitia risiti zote unapoletewa taarifa. Kagua zote na hatimaye
ufunge taarifa yako.
2.
Nunua kaunta ‘book’ kwa ajili ya kutawala vitabu vyote. Unapopokea
vitabu ofisini hakikisha unahakiki namba zote kuwa ziko sawa. Pia
unapotoa kitabu hakikisha unamsainisha anayepokea kwa kuandika jina
lake, cheo chake kanisani, na tarehe na namba ya kitabu kinachorudi
hatimaye namba ya kitabu kinachotoka. Epuka kutoa kitabu kingine bila
kupokea kinachoisha.
MAMBO YANAYOMHUSU MKE WA MCHUNGAJI MPYA.
Kazi na mafanikio ya mchungaji ipo
nyuma ya mke wake na hata watoto wake. Mwenzi wako anaweza kuifanya
kazi yako kuwa ngumu awe rahisi kwa namna anavyohusiana na washiriki.
Ikiwa atakuwa mgomvi kila wakati kazi yako itakuwa chungu katika kila
mtaa utakaokwenda. Hivyo mama mchungaji anapaswa kuwa mwangalifu sana
katika kuisimamisha kazi ya Mungu katika mtaa au mazingira yao.
1. Mke wa mchungaji usiwe na rafiki unayempendelea mtaani au ofisini.
2.
Mke wa mchungaji epuka kumsema mke wa mchungaji au mchungaji
aliyeondoka kabla yako. Usikubali kumsengenya kwa njia yoyote.
3.
Mke wa mchungaji na kwaya ya kanisa. Hakuna ubaya kuwa mwimbaji wa
kwaya ya kanisa. Bali tatizo ni pale mke wa mchungaji unaposhindwa
kutambua kuwa wewe ni mwimbaji lakini kubwa kupita yote ni mke wa
mchungaji. Epuka vikao vya kwaya na mambo ya kwaya yanayoleta upinzani
na kanisa au kufanya kinyume na maadili ya kanisa. Uwe na tahadhari
katika ushiriki wako katika kwaya maana ni kitendo nyeti ambacho mara
zote kinaangaliwa kwa umakini sana (sensitive area).
4.
Mke wa mchungaji unapaswa uwe kielelezo katika kuvaa kwako, kujipamba
kwa kiasi, na mazungumzo yako. Kumbuka kazi ya mchungaji inakuwa nzuri
au mbaya pale mke anapokuwa na mvuto mzuri au mbaya. Omba sana maana
Shetani anaweza kukufanya kikwazo cha kazi ya Mungu.
5.
Mke wa mchungaji jiepushe kujiingiza katika migogoro inayomhusu mume
wako dhidi ya washiriki. Kunapotokea kutokuelewana kati ya mchungaji na
uongozi au kanisa kazi yako uliyopewa na Mungu sio kuchochea magomvi
bali ni KUOMBA NA KUMFARIJI MUMEO.
No comments:
Post a Comment