Blogger Widgets FURSA KWA VIJANA WOTE TUPAMBANE KWA KILA NJIA ILI MRADI TUWEZE KUEPUKA HUU UMASKINI TANZANI NA AMIN KILA ATAFUTAYE KWA NIA HUPATA MAANA ATA MAANDIKO HUSEMA PENYE NIA PANA NJIA

Thursday, October 16, 2014

PAMOJA NA UTAMU WAKE, UKIMCHUNGUZA KUKU HUMLI!

Habari gani waungwana na wadau wa ukurasa huu. Nina uhakika mambo yenu yanakwenda vilevile mlivyopanga, maana maisha bwana ni vile mtu unavyopanga. Ukitaka kuwa msumbufu kwa waume za watu unaweza, ukitaka kuwa kiwembe kwa wake wa wenzio pia waweza, umeona bwana?
Juzikati nilipata simu moja ya kushangaza kidogo kutoka kwa mmoja wa wasomaji wa safu hii. Yeye ni mdada, aliniambia ana tatizo kubwa ambalo hajui namna ya kulikabili, eti kila akimpata mwanaume baada ya muda mfupi anamtosa. Nilitegemea angeniambia kila baada ya muda anaachwa, eti sasa yeye ndiye anayewatosa.
Nikajua labda kicheche, nikamuuliza kwa nini, hapo ndipo akaniacha hoi kabisa. Eti, yeye anajua sana kupenda, lakini ana wivu wa kupitiliza. Yaani akiwa na mwanaume hataki achepuke, kwa hiyo anaikagua simu yake mara kwa mara na anapohisi kutendwa tu, anampiga chini. Kwa mujibu wa maelezo yake, amewaacha wengi sana!
Kisa chake kimenifanya nimkumbuke kuku, huyuhuyu wa kitoweo. Ninataka kuchukulia mfano wake ili kukuwezesha wewe msomaji wangu kuungana na mimi katika kumshauri huyu mdada, aliyetamba kuwa kutokana na urembo wake, hakaukiwi wanaume!
Sijui kwa wengine, ila kwangu mimi kuku ni moja kati ya vitoweo vitamu ninavyovipenda, baada ya hapo kuna hii nyama ya Swala, dah, aisee, ni tamu sana. Lakini unazijua tabia za kuku?
Chakula anachokula kuku, kama wewe ni mtu wa kumaindi, walahi huwezi kumla. Kuku anakula kinyesi cha binadamu, tena anakishambulia kwa furaha kwelikweli. Yaani, kuku akikuta mzoga wowote, anakula, tena vizuri tu na akitoka hapo anatafuta maji ya kunywa.
Kuku akimkuta chura, anamla kama hana akili nzuri. Tena anafanya hivi siyo kwa kujificha, hadharani kabisa. Unaweza kumkuta kwenye kakichana anafurahia msosi, ukienda unamkuta anakula vitu yaani hadi daah!
Vitu vyote hivi anavyokula kuku, kwetu sisi ni kinyaa. Unajua kwa nini tunamla? Tunamla kwa sababu hatumfuatilii wala kutilia maanani kama anakulaga hivyo vitu. Sisi tukimfungulia asubuhi kutoka bandani, hatuna time naye, tunasubiri jioni aingie tumfungie, uongo?
Ndivyo unavyoweza kumfananisha na mpenzi wako, awe wa kike au wa kiume. Usimfuatilie, utakosa uhondo. Nilimwambia yule dada na najaribu kurudia tena hapa, ni nadra sana, yaani sana, kumkuta mtu kamili katika mapenzi.
Sihamasishi watu wachepuke, lakini ni lazima niwe mkweli, kuna watu wachache sana miongoni mwetu ambao ni waaminifu kwa asilimia zote katika uhusiano wa kimapenzi. Wengi, hata wale walio katika ndoa, wana mtu wa nje wanashughulika naye!
Kinachompasa mtu kufanya ni kujenga imani kwa mwenzake kwamba hachepuki. Acha kukagua simu yake. Wapo baadhi ya wenza, mwenzake akifika tu, kitu cha kwanza ni kuanza kucheza na simu yake, sms gani zipo, simu gani zimeingia, zipo zimetoka kwenda wapi.
Ni kwamba, hapo anatafuta kuipata sms atakayoitilia shaka. Mwenzake akitoka kwenda kazini au kwenye mitikasi mingine ya maisha, mwenza wake yuko nyuma anajifichaficha, anataka aone amesimama na nani, anakwenda wapi!
Niwaambie ukweli kuwa kumfuatilia mwenza wako ni kujipa presha, stress na machungu yasiyo na sababu. Atasimama na mtu wa kazini kwao, utaamini ni mpenzi wake, atazungumza na mtu simuni, utaamini ni wake.
Lakini siyo tu kujipa stress, wakati mwingine ni kujiumiza hasa utakapogundua kuwa ni kweli mwenzako anakusaliti. Asikudanganye mtu kuwa dawa ya msaliti ni kuachwa, utaacha wangapi? Jiweke mbali na vitu vinavyoweza kukuongoza kujua yanayofanywa na mwenzako na kila mara, jitahidi kujiepusha na kitu chochote kinachoweza kumpa mashaka mwenzako kuhusu maisha yako ya kimapenzi.

No comments:

Post a Comment

TUPAMBANE BLOG