Blogger Widgets FURSA KWA VIJANA WOTE TUPAMBANE KWA KILA NJIA ILI MRADI TUWEZE KUEPUKA HUU UMASKINI TANZANI NA AMIN KILA ATAFUTAYE KWA NIA HUPATA MAANA ATA MAANDIKO HUSEMA PENYE NIA PANA NJIA

Friday, December 19, 2014

Epuka kuchunga mifugo kwenye maeneo hatarishi

Licha ya kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozalisha mifugo ya aina mbalimbali na kwa wingi kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo lakini inakabiliwa na upungufu mkubwa wa maeneo ya ufugaji sambamba na malisho ya kutosha kwa ajili ya mifugo hiyo.


Mbuzi barabaraniWafugaji walio wengi, wameshindwa kukabiliana na changamoto hizo hasa kwa kutenga maeneo maalum ya kuchungia au kufuga majumbani, na badala yake wanalazimika kuchunga mifugo hiyo katika maeneo hatarishi na yasiyofaa kwa shughuli hizo.

Maeneo hatarishi ambayo mara nyingi yamekuwa yakitumika kwa ajili ya kuchungia mifugo ni pamoja na pembezoni mwa barabara zinazopita vyombo vya moto kama magari, kwenye maeneo ya migodi, kwenye mashimo makubwa yaliyotokana na uchimbaji wa mawe, na hata katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kutupa taka bila kujua madhara yanayoweza kuikabili mifugo yao.


Madhara yanayotokana na kuchunga katika maeneo hatarishi


eneo hatarishiMajalala
• Mifugo inapochungwa katika maeneo yanayotumika kutupa taka hula makaratasi, au nailoni ambazo huharibu mfumo wa chakula na kuzuia mfumo mzima wa umeng’enyaji.
• Mifugo huweza pia kula vitu vilivyotupwa vyenye sumu ambazo huharibu mfumo wa chakula vile vile na hata kusababisha vifo.
• Wanyama huweza kuchomwa na vitu vyenye ncha kali kama vile vyuma wakiwa katika harakati za kula. Vyuma hivyo vinaweza kuwadhuru kwenye miguu au hata mdomoni wakati wa kula na kuwajeruhi hata kupelekea kifo kutokana na kuwa vitu hivyo wakati mwingine huweza kuwa na sumu ambayo huleta madhara kwenye mwili wa mnyama.


Migodini
• Mifugo inapochungwa katika maeneo ya migodi au pembezoni mwa migodi kwa mfano migodi ya dhahabu, huweza kula sumu (mercury poison) inayotokana na maji yaliyotumika kusafishia dhahabu.
• Sumu hiyo huharibu mfumo wa neva (nervous system) na huweza kusababisha mnyama kufa.


Maeneo yenye mashimo makubwa

• Mifugo inapofugwa kwenye maeneo yenye mashimo makubwa hasa yaliyotokana na uchimbaji wa mawe huweza kuumizwa na wanyama wakali kama vile nyoka ambao huwadhuru mifugo na kusababisha madhara makubwa mwilini na hata kusababisha mnyama kufa.
• Ikiwa wanyama wanachungwa katika maeneo ya mashimo makubwa huweza kuanguka na kuvunjika miguu na hata kupoteza uhai.
• Wakati mwingine mifugo huweza kupotea. Mfano; ndama wanaweza kuachwa wakiwa wamelala na wasijue kama mifugo mingine imehama na kwenda eneo lingine au wakati mwingine wakatumbukia kwenye mashimo na wasiweze kutoka.



Barabarani
• Mifugo kama itachungwa katika maeneo ya barabarani kunakopita magari, pikipiki na baiskeli huweza kupata ajali kwa kugongwa na hatimaye kuumizwa vibaya na hata kusababisha kifo.
• Majani yanayopatikana pembezoni mwa barabara yanapotumiwa na mifugo kama chakula huweza kuwadhuru kwani yana sumu (lead poison) ambayo hutokana na moshi wa vyombo vya usafiri. Ng’ombe anapokula majani hayo hupata matatizo kwenye mfumo wa neva na unaosababisha kupata upofu na kupoteza nguvu na hatimae kufa.


Mambo ya kufanya kuepukana na hayo;

• Kabla ya kuanza kufuga ni muhimu mfugaji ukatambua eneo ulilo nalo na
kiasi cha mifugo utakaoweza kuwafuga katika eneo hilo.
• Hakikisha eneo hilo litatosha kulisha mifugo yako hivyo hautohitaji kwenda kuchunga mifugo katika maeneo hatarishi kwa lengo la kukidhi lishe na kuwe na uwiano wa eneo na mifugo.
• Hakikisha unakuwa na malisho ya kutosha kwa wakati wote wa kufuga.
• Jenga mazoea ya kulisha mifugo yako nyumbani.
• Kata majani na wapatie wanyama katika mabanda uliyoandaa kwa ajili ya kulishia.
• Ikiwa utalazimika kutafuta malisho kwa ajili ya mifugo, basi epuka kuchunga
katika maeneo hatarishi, ni vyema ukachunga kwenye mashamba yaliyokwisha kuvunwa vyakula au katika maeneo maalumu yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya kulishia.
• Ni muhimu kutenga malisho maalumu ya mzunguko. Kuwa na maeneo mbalimbali kwa ajili ya kulishia kwa nyakati tofauti. Hii itasaidia kukidhi chakula cha mifugo hata wakati wa ukame.

No comments:

Post a Comment

TUPAMBANE BLOG