Blogger Widgets FURSA KWA VIJANA WOTE TUPAMBANE KWA KILA NJIA ILI MRADI TUWEZE KUEPUKA HUU UMASKINI TANZANI NA AMIN KILA ATAFUTAYE KWA NIA HUPATA MAANA ATA MAANDIKO HUSEMA PENYE NIA PANA NJIA

Monday, December 1, 2014

KUNA UMUHIMU WA KUPEKUA SIMU YA MPENZI WAKO?-2


“Ndugu mwandishi, nakupongeza kwa mada yako nzuri lakini nasikitika kwamba umeandika kwa kuegemea upande mmoja tu. Ni kweli siyo vizuri kupekua simu ya mwenzi wako lakini je, pale unapopekua na kufuma meseji za mapenzi kwenye simu ya mwenzi wako, nani mwenye makosa? Wewe uliyepekua au yeye anayekusaliti?”
Nimeamua kuanza kwa staili tofauti leo, huo hapo juu ni ujumbe nilioupata kutoka kwa msomaji wangu mmoja baada ya kuwa amesoma mada tuliyoanza nayo wiki iliyopita. Mwitikio nilioupata wiki iliyopita, ulikuwa mkubwa sana kutoka pande zote mbili, wanaume na wanawake. Wanaume wengi walionesha kuifurahia mada, wengi wakawa wanatoa ushuhuda wa jinsi walivyoamua kuzikatisha ndoa zao au jinsi wanavyogombana na wenzi wao kila siku, chanzo kikiwa ni simu.
Kwa upande wa wanawake, walionekana kukasirishwa na mada hii kwa maelezo kwamba imeelemea upande mmoja tu, kuwakandamiza wanawake!
SIMU NI TATIZO KUBWA KWENYE MAPENZI
Kutokana na maelezo ya pande zote mbili, nilichojifunza ni kwamba matumizi ya simu za mkononi yamegeuka na kuwa tatizo kubwa kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Ni kama kansa ambayo taratibu inazitafuna ndoa za watu wengi, inavuruga uhusiano wa kimapenzi wa maelfu ya watu na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, ndivyo tatizo linavyozidi kuwa kubwa.
Simu zinaonekana kuwa kichaka cha kurahisishia usaliti, wanandoa wengi wanalia baada ya kugundua uozo mkubwa kwenye simu za wenzi wao. Kwa maelezo ya baadhi ya wasomaji wangu, hasa wanawake, wanaume wengi wanatumia vibaya simu zao na kwamba njia pekee inayoweza kuwasaidia kuujua ukweli, ni kuendelea kuzipekua kadiri iwezekanavyo.
NINI CHA KUFANYA?
Kama nilivyoeleza hapo juu, wanawake wengi wanasema kuna umuhimu wa kuendelea kupekua simu za wapenzi wao na kwamba njia hiyo inawasaidia kuwabaini wezi wao mapema hivyo kuwa katika nafasi nzuri za kuzilinda na kuzitetea ndoa zao.
Wanaume nao wanasema ni makosa makubwa kwa wanawake wanaoishi nao kimapenzi kupekua simu zao kwani wanawaharibia ‘madili’ yao. Yaani ni kama ule usemi usemao ‘kila mwamba ngoma huvutia kwake’.
Hata hivyo, kwa kuwa lengo letu siyo kubishana bali kuelekezana mbinu za kupunguza migogoro katika uhusiano wa kimapenzi, ni vizuri tukafikia muafaka ambao utakuwa na maana kwa pande zote mbili.
SIYO KOSA KUSHIKA SIMU YA MWENZI WAKO
Kwa watu ambao wanaishi katika uhusiano wa kimapenzi wenye uaminifu wa hali ya juu, hakuna tatizo lolote kwa mwenzi wako kushika simu yako. Hujawahi kuona mume na mke wanabadilishana simu hata kwa siku nzima na hakuna tatizo lolote linalotokea? Kama bado hujaona, wapo, tena wengi tu na mimi ni shahidi wa hilo.
Hata hivyo, hilo linawezekana kama tu kila mmoja atakuwa mwaminifu kwa mwenzake. Unaogopa nini mwenzi wako kushika simu yako wakati huna michepuko? Huna mtu atakayekutumia meseji za mapenzi wala kukushukuru kwa mapenzi au zawadi ulizompa jana?
Ukiwa mwaminifu, hutakuwa na haja ya kuweka ‘password’ kwenye simu yako, kuificha wala kulala nayo ikiwa chini ya mto kwa kuhofia mwenzako asisome meseji. Hutasikia mwenzi wako akimtumia meseji za matusi mtu anayewasiliana na wewe hata kama ni mwanamke kwa sababu haya yote yanakuja baada ya kuona mazingira yenye harufu ya usaliti.
Ukiwa mwaminifu kwa mwenzi wako, wala simu siyo tatizo na hutakuja kugombana na mwenzi wako ila ukiendekeza michepuko, kila siku mtakuwa mnagombana.

No comments:

Post a Comment

TUPAMBANE BLOG