Blogger Widgets FURSA KWA VIJANA WOTE TUPAMBANE KWA KILA NJIA ILI MRADI TUWEZE KUEPUKA HUU UMASKINI TANZANI NA AMIN KILA ATAFUTAYE KWA NIA HUPATA MAANA ATA MAANDIKO HUSEMA PENYE NIA PANA NJIA

Thursday, February 5, 2015

Wakala wa chakula yahamasisha kilimo cha mahindi



KILIMO cha zao la mahindi kimeendelea kuonekana kama ni njia mbadala ya kumkomboa mwananchi wa kawaida na hasa kwa mikoa ya nyanda za juu Kusini, lakini pia ushiriki wa karibu wa Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (National Food Reserve Agency (NFRA), kumechangia kuongeza hamasa katika sekta hiyo muhimu kwa maisha na maendeleo ya wananchi na hasa wa vijijini.
Nilitembelea mikoa hiyo na nikaangazia kilimo hicho kwa mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya, inayofahamika kama kanda ya Makambako ya NFRA, inayohuduma wilaya za Njombe, Ludewa, Makete, Wanging’ombe, mkoani Njombe na wilaya za Mbarali, Mbeya, Chunya, Ileje na Mbozi, katika mkoa wa Mbeya.

Kwa kuanzia nilikutana na Meneja wa Kanda hiyo, (Makambako Zonal Manager) Abdillah Nyangassa, ambaye pamoja na mambo mengine alitoa ufafanuzi kuhusu hali ya soko la mwaka 2013/2014 na mafanikio yake kwa wakulima.

Licha ya kuwepo kwa changamoto za hapa na pale, Nyangassa, anasema NFRA kama chombo cha serikali, hakifanyi kazi zake kisiasa na kimeweza kufikia malengo yake kulingana na bajeti ya fedha zinazotengwa na serikali kwenye bajeti.

Kilimo cha mazao ya chakula na biashara ni moja kati ya nguzo muhimu kwa maisha ya wananchi wa mikoa inayohudumiwa na kanda ya Makambako ni sejemu ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, awali ilipewa jina la The Big Four, likimaanisha mikoa yenye nguvu za uzalishaji mkubwa kwa mazao ya chakula.

Kanda ya Makambako yenye vituo vya Vwawa wilaya ya Mbozi, Isongole wilaya ya Ileje mkoa wa Mbeya, ambako uzalishaji wa mahindi umekuwa mkubwa na unaoongezeka kila siku hivyo kuwapo kwa ziada ya chakula kwa familia hununuliwa na serikali kwa ajili ya akiba ya Taifa kupitia NFRA.

Aidha, NFRA kanda ya Makambako, kwa mujibu wa Nyangassa, hutumia vituo vya Igwachanya katika wilaya ya Wanging’ombe, Shauri Moyo, Mawengi, Mlangali, Ludewa Kijijini, wilayani Ludewa, lakini ni vituo maalum vinavyotumika kwa ajili ya ununuzi na uhifadhi kwa muda tu.

Pia hukitumia kwa ajili ya manunuzi na uhifadhi mahindi hayo Kituo kikuu cha Kanda hiyo kilichopo katika mji wa Makambako wilayani Njombe, mkoani Njombe, ambako pia kuna maghala makubwa ya kuhifadhia chakula, lakini pia utunzaji baada ya kupulizia dawa hufanyika kwa ustadi mkubwa, ili kuondoa wadudu waharibifu wa mazao.

Hata hivyo, Nyangassa, anasema bayana kuwa wakulima wanaitegemea kwa kiasi kikubwa NFRA katika kufikia malengo ya kilimo, kwa maana ya kuongeza tija na uzalishaji pamoja na mavuno, huku akisisitiza bajeti kwa ajili ya wakala hiyo inafanywa kulingana na uwezo wa kuhifadhi chakula.

Anasema NFRA imefanikiwa kununua ununuzi katika vituo vilivyopo katika wilaya ya Ludewa kiasi cha zaidi ya tani 2,500 za mahindi ya wakulima, SACCOS, AMCOS na vikundi maalum na ambavyo tayari vimetambuliwa na NFRA vya wafanyabiashara, ambapo kulingana na takwimu za wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika za mwaka 2010/2011, zaidi ya watu milioni 8.6 wanakitegemea kilimo cha zao la mahindi katika mikoa inayohudumiwa na kanda ya Makambako.

Nyangassa anasema ya kwamba msimu wa ununuzi wa mwaka huu, NFRA imetumia SACCOS na AMCOS, kwa nia ya kushiriki kufufua ushirika na kuwa tayari wilaya za Ileje, Mbozi, Wanging’ombe, Ludewa na Njombe, zimeanzisha mwendo.

“Ni safari ya kuelekea kuviwesha vikundi vya wakulima, na hii ndio lengo kuu la kuongezesha ushawishi kwa wakulima kujiunga katika vikundi vya ushirika au vikundi jamii, kwani wanaweza kupitia njia hiyo hata misaada ya serikali ya mafunzo ya kilimo bora na hata kuwezeshwa,” alisema Nyangassa.

Hata hivyo, Nyangassa, anasema ya kwamba, mpaka zoezi la ununuzi linasitishwa, bado kuna baadhi ya wakulima wenye mahindi majukumbani, akisema hatua hiyo ilitokana na wengi kudhani kuwa bei ya Sh. 500 kwa kilo moja ya mahindi iliyokuwa ikitumika baada ya kufunguliwa kwa soko, inaweza kuongezeka.

Kulingana na Nyangassa, katika kituo cha ununuzi cha NFRA cha Mawengi kinachounganisha vijiji vya Mbwila, Kiwe, Madunda, Lupande na Mawengi yenyewe, kuna malalamiko kwamba kuna kiasi kikubwa cha mahindi ya ziada kilichobaki kwa wananchi, lakini akasema hatua hiyo inalenga kuweka tahadhari kwa jamii.

“Unajua wakulima na wananchi wakiliona soko zuri kama lilivyo la NFRA, wangehitaji kuendelea kuuza mazao yao, lakini kitu kikubwa na cha muhimu ni kwamba NFRA inanunua ziada ya chakula hicho na wala sio mavuno yote ya msimu,” anasema Nyangassa.

Anasema ili kutambua hali ya mavuno, NFRA huwatumia watendaji na wenyeviti wa vijiji na vitongoji katika kupata taarifa sahihi, ili kuondokana na dhana ya kufunguliwa kwa vituo kisiasa hatua ambayo baada ya muda mfupi hufuatiwa na malalamiko ya upungufu mkubwa wa chakula na njaa.

“Tunafanya hivyo huko Mlangali, kwa kuwatumia viongozi kama Paschal Mayumbwa, mwenyekiti wa kitongoji cha Mlangali Ndani, Renato Kahako Willa, mwenyekiti wa kijiji cha Mawengi, Adriano Mwinuka, wa kijiji cha Shauri Moyo, na wengine ili kujua hali halisi ya mavuno,” anasema Nyangassa.

Alhaji Nyangassa, alisema kwamba baadhi ya vijiji wilayani humo vimekuwa na kasi ya uzalishaji wa mahindi mwaka hadi mwaka, ikiwa ni pamoja na Shauri Moyo, Ludewa, Mawengi na Mlangali, lakini hiyo inatokana na uhakika wa soko la NFRA.

“Kwa hakika wakulima wengi wanafanya hivyo kwa nia ya kulikimbia soko la walanguzi ambao hivi sasa wako tayari na wanazunguka katika maeneo ya vijijini wakitaka kununua mahindi hayo kwa bei ndogo, ambayo kwa kweli haina msaada na manufaa kwa mkulima,” anasema Nyangassa.

Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe, DC Esterina Kilasi, aliliambia gazeti hili kwamba kazi nzuri inayofanywa na NFRA ndiyo inayochochea kasi ya wananchi kuongeza maeneo ya kilimo cha mahindi kwenye wilaya yake.

“Wakulima wetu wameanza kuona fulsa muhimu za kushiriki kilimo cha mahindi na hili ni kutokana na kuwapo kwa uhakika wa soko la mahindi la NFRA kanda ya Makambako, binafsi kama sehemu ya serikali nimefarijika, na ninawapongeza watendaji hao kwa kazi nzuri na ya kupigiwa mfano” alisema DC Kilasi.

Mkuu huyo wa wilaya, alisema mbali na kufarijika kwa uhakika wa soko hilo la serikali, lakini pia ukaribu na utaratibu mzuri wa NFRA kufungua masoko katika vijiji vya Igwachanga na Igalala ndani ya wilaya yake.

“Wakulima wengi sasa wameanza kuona umuhimu wa kuwepo kwa serikali na hasa baada ya kufunguliwa kwa masoko kwenye vijiji vyao, badala ya hapo awali ambapo walilazimika kulifuata kwa umbali mrefu soko la NFRA au la wanunuzi wengine,” alisema DC Kilasi na kuongeza kuwa hatua hiyo imepunguza adha ya walanguzi kuwalaghai wakulima.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Ludewa, DC Juma Madaha, alisema kuwa NFRA imeisadia serikali kupunguza malalamiko ya wakulima hasa wanapokosa soko la uhakika la mazao yao, licha ya kuwapo kwa hamasa kubwa.

“Tunatumia muda mwingi kupita vijijini kwa ajili ya kuhamasisha wakulima na hasa vijana kuendelea kushiriki katika kilimo, hivyo ni matarajio yetu kuwapo kwa uhakika wa soko la mazao hayo,” alisema DC Madaha.

Mkuu huyo wa wilaya alisema fulsa pekee ya wazi kwa mkulima wilayani humo ni kuona vituo na masoko ya NFRA yanayozunguka kwenye maeneo ya vijijini, (mobile buying centers), na kuongeza kwamba mfumo huo umewapunguzia usumbufu wananchi.

Baadhi ya wakulima wa mahindi akiwamo Agnes Mkinga, wa kijiji cha Mawengi, wilayani Ludewa, alisema na kuishukuru NFRA kanda ya Makambako kuchukua maamuzi ya kufungua vituo vya ununuzi kwenye maeneo ya vijijini ambapo pia ilitangaza bei ya msimu kuwa Sh. 520.

Mkinga alisema hatua hiyo ya kutangaza bei nzuri iliwafariji wakulima kwa kiasi kikubwa, lakini wengi walikuwa hawajamaliza kuvuna mahindi yao, hivyo mpaka vituo vinafungwa kutokana na kufikiwa kwa malengo ya ununuzi bado kulikuwa na kiasi kikubwa cha mahindi.

“NFRA imefanya mambo makubwa kwa wakulima wa mahindi, na kwa hakika mahindi yakiwekewa mkazo, yanaweza uhamasishaji kama ambavyo Rais Jakaya Kikwete, alivyosema wakati alipokuja kwenye ziara na uzinduzi wa mkoa mpya wa Njombe, kwamba mazingira yakiboreshwa kilimo cha mahindi kitakuwa mkombozi wa maisha ya wananchi wengi zaidi lakini pia akitaka kuondokana na uvivu” alisema Mkinga.

Wakulima wengine pamoja na kuishukuru Serikali kwa majukumu ya uhakika yanayofanywa na NFRA, lakini walishauri wakala hiyo kuongezewa majukumu ili kulihudumia zao la mahindi kama kweli nia ni kuona tija.

“Lakini pamoja na mambo mazuri na hasa kwenye kununua mahindi, sasa ni vyema NFRA ikapewa na serikali majukumu ya kusambaza mbolea kwa wakulima na hasa kwenye maeneo yenye vituo vya ununuzi,” alisema Michael Komba, mkazi wa Ludewa.

“Kuja na kununua mahindi ya wakulima kwa ajili ya hifadhi ya Taifa bila kuiwezesha NFRA kujenga mtandao usiokuwa na shaka ya wapi kumepatikana mavuno mengi katika msimu sio matumizi bora ya rasilimali na yenye tija,” alisema mkulima Hilda Mgaya.

Mkulima huyo alisema kukosekana kwa pembejeo za uhakika na hasa kutoka katika ofisi za serikali, kumechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa wauzaji wa mbolea feki inayoangamiza ardhi na kudumaza mavuno ya mazao.

“Lakini pia kukosekana kwa soko la muda mrefu kwa maeneo ya vijiji kamwe hakukidhi haja ya kilimo, kwani mwaka jana mahindi mengi yalikosa ubora na yaliozoea kwenye nyumba za wananchi, hivyo pamoja na serikali kutakiwa kuongeza fedha, lakini pia kuipa NFRA jukumu la kusimamia mbolea vijijini,” alisema Hilda Mgaya.

Mwenyekiti wa Muungano wa vikundi vya wakulima wadogo wa mahindi katika wilaya za Iringa Vijijini na Kilolo,  Yohanes Mhanga, alisema kwamba japo soko la NFRA ni la uhakika kwa mkulima, lakini bado lipo mbali na maeneo yao ya kilimo.

Mhanga alisema ya kwamba soko hilo la NFRA limesaidia kuwaongezea ujasiri wakulima wengi wa vijijini waliokuwa wakihujumiwa na baadhi ya wafanyabiashara na walanguzi, kukabiliana na hali hiyo kwa kuikimbilia wakala hiyo.

Mhanga alisema ni vyema serikali ikakubali kuongeza fedha ili kuipatia nguvu na uwezo NFRA, kufanya utafiti wa hali ya chakula nchini, badala ya kutumia taarifa nyingi za mezani za maafisa kilimo wa wilaya.

“Maafisa wengi hawaendi vijijini, wanafanya makadirio ya kimazoea, lakini wananchi wengi wanalima na wanavuna mahindi mengi, lakini kwa vile wao wanaendelea na majukumu yao ya kimazoea, NFRA bado haijaliona eneo letu kama lenye uzalishaji mkubwa wa mahindi,” alisema Mhanga.

Mmoja wa wakulima wakubwa wilayani Mbozi, Jeremiah Isso, aliliambia gazeti hili katika mahojiano maalum kwamba NFRA tayari imesaidia kwa kiasi kikubwa kuwajengea ujasiri wa kiuchumi na kuwakomboa wakulima wengi.

“Leo mkulima wa mahindi anatambiana na mkulima wa pamba, kahawa na hata tumbaku, na hii ni kutokana na uhakika wa soko la NFRA, hivyo naiomba serikali ifanye mapinduzi makubwa ya kibajeti kwa kuiangalia NFRA ambayo sasa inahudumia wananchi vijijini,” alisema Isso.


Mratatibu wa shughuli za kilimo cha mahindi katika wilaya ya Ileje, Deogratius Mtewele, alisema kilimo cha mahindi kimeendelea kuwa mkombozi kwa wananchi wengi, lakini pia akishukiuru NFRA na wizara ya kilimo kwa kuwathamini wananchi.

Mtewele alisema kwa mara ya kwanza NFRA mwaka huu imetoa bei nzuri na ambayo imewafariji watu wengi, lakini pia matumizi ya Soko la Kimataifa la Isongole, kama kituo cha ununuzi.

“Kwa kweli tumefarijika na NFRA, lakini pia matumizi ya soko hili la Isongole, lililojengwa kwa nguvu za wananchi wa nchi mbili za Malawi na Tanzania, nalo limeendelea kuwa kivutuo muhimu cha ununuzi wa mahindi ya wakulima wa wilaya hiyo na maeneo ya jirani,” alisema Mtewele.

No comments:

Post a Comment

TUPAMBANE BLOG