MAPENZI HUWA IMARA PALE YANAPOJENGEWA NJIA YA KUTOKA NA KUINGIA -3
MPENZI
msomaji, naendelea kuelezea ‘topiki’ inayoelezea namna mapenzi
yanavyokuwa imara yakijengwa. Tuwe pamoja hadi nitakapoishia.
Mwenzi
wako atakuheshimu mno kama nawe unamuonesha utiifu. Hata wasaliti
wengi, wamejikuta wakisalitiwa baada ya kuwaonesha wenzi wao jinsi
wasivyo waaminifu.
Onesha
utu ili uendelee kufaidi upendo na huduma. Mwenzi wako amekuwa akitumia
fedha nyingi kukuhudumia, jambo unalodaiwa kwake ni utu.
Hakikisha unampa faraja mpaka hajutii kile anachokitoa kwake. Faraja siyo mapenzi ya kitandani peke yake.
Unapaswa
kutuliza akili na ujue mwenzi wako anahitaji nini kutoka kwako.
Ukishakifahamu, ni juhudi yako kuhakikisha hakikosi. Kufanya hivyo ndiyo
utu na ndivyo utakavyoweza kumteka zaidi na zaidi. Atakapokuwa
anakutendea lakini maombi yake huyapokei vizuri, unakuwa unamkatisha
tamaa.
Kadiri unavyomkatisha tamaa ndivyo unavyoelekea kumvunja moyo.
Tambua kwamba moyo unapovunjika inakuwa ni ngumu mno kuurejesha kwenye
hali yake ya kawaida. Kwa maana hiyo unakuwa umepoteza upendo na huduma
zote ulizokuwa unazipata kutoka kwake.
Mapenzi ni mchezo wa nipe
nikupe. Nipe upendo na wewe nikupende. Inawezekana yeye ndiye alianza
kukupenda ndiyo maana akafanya juu chini mpaka mkawa pamoja. Baada ya
hatua hiyo ni muhimu kwako kuhakikisha unaonesha upendo kwa sababu
mmekubaliana kupendana.
Kupenda siyo maigizo, kusema utamfanyia
magirini mwenzi wako ili utimize matakwa yako fulani. Kila aliyeingia
kwenye uhusiano kwa malengo tofauti na upendo alifeli. Unaposoma makala
haya, ikupe njia nzuri ya kutimiza wajibu wako kwenye mapenzi halafu
umuache naye atimize kwa upande wake.
Unapokuwa unatimiza wajibu
wako, hebu jiulize naye anafanya nini? Ni hatari sana kuendelea kuonesha
unampenda na kumjali, wakati yeye hakujali kwa chochote. Mapenzi siyo
tu kwamba yapo, ila yamekuwepo kwa ajili ya kupeana faraja.
Kama
mwenzi wako hakufariji maana yake unatakiwa uhame hapo ulipo. Jinsi
utakavyokuwa unazidisha upendo, haitakusaidia, kwani ni sawa na kumpigia
mbuzi gitaa. Badala ya kukushukuru, yeye atakuona zezeta uliyekufa
kwake. Unatakiwa kuutetea moyo wako.
Naomba nikushauri kuwa akili
yako iwe hai kila siku. Uwekezaji wako uendane na kile ambacho wewe
unakipokea kutoka kwa mwenzi wako. Kufanya zaidi au pungufu ni kosa
kubwa. Kufanya zaidi maana yake unakuwa unaunyanyasa moyo wako na
pungufu unakuwa humtendei haki mwenzio.
Labda nisisitizie kitu. Sina
maana kwamba kama wewe unatoa fedha ni sharti naye awe anakupa, la
hasha! Uhusiano bora wa mapenzi huboreshwa na namna ambavyo wahusika
wanavyohudumiana. Kila mmoja kuhakikisha anakuwa jirani na mwenzake
wakati wote.
Mmoja anaweza kuwa na matatizo ya kipato, ni vizuri sasa
mwenzake kuwa naye karibu kuhakikisha changamoto hiyo inakwisha. Ni
ajabu pale mtu anapokabiliana na hali ngumu ya muda mfupi na anahitaji
tu faraja kutoka kwa mwenzi wake lakini akawa hapati.
Hizo ndiyo
dalili za unyonyaji. Kama wewe matatizo yako ya kifedha unayaweka mstari
wa mbele na unatatuliwa, iweje mwenzako umeshindwa kumfariji wakati wa
shida zake? Hiki ni kipengele kibaya ambacho kimewafelisha wengi. Baadhi
wamepoteza wapenzi bora kwenye maisha yao.
No comments:
Post a Comment