Simulizi inayogusa maisha yako na jamii inayokuzunguka
Ilipoishia...
**** “Rudi kitandani Malaya we! Ukileta mchezo nakuua” Masharubu alimkaripia Ashura huku akiuchukua tena mkanda wake, alimchapa Ashura, Ashura hakuweza kuvumilia tena alinyanyua chupa ya kubwa ya dompo na kumpiga Pedeshee kichwani, Perdeshee aliyumba na kuanguka chini, kabla hajakaa sawa alikutana na chupa ya konyagi iliyopasukia usoni, Pedeshe Masharubu alichanika vibaya usoni na kichwani, damu zilitiririka na kuchafua shati lake alilovaa, alitulia kimya sakafuni. ‘Nimeua, mama yamgu mimi’, Ashura alijililia moyoni huku mkono wake mmoja kajishika kichwani na mwingine akiupigapiga. Kwa haraka alivaa gauni lake hakukumbuka nguo nyingine, akauendea mkoba wa Pedeshee alipoufungua alikuta maburungutu ya noti yamejifungafunga, akatetemeka sana afanyeje, achukue moja nyingine amuachie, au abebe begi zima, swali halikuwa na jibu, akabaki mdomo wazi.
endelea...
Alitazama uku na huku kama kuna mtu mwingine anayemuona, alisahau kama yuko chumbani. Aliingiza mkono katika begi lile na kutoa bulungutu moja na kuyaacha mengine, akauendea mlango ili atoke nje. Alipofika mlangoni alisikia sauti za watu wakija upande huo huku wakiongeaongea aliogopa sana, akasubiri kidogo, akatazama tena begi lile ‘utajilaumu baadae’ sauti ya ndani ilimwambia. Akaona ujinga, alirudi na kuchukua begi zima kisha akatoka kana kwamba hakuna tatizo. Alitembea hatua za haraka haraka na kuziendea ngazi ambazo zilimpeleka mpaka chini, alipofika mapokezi hakuangalia mtu moja kwa moja alitoka nje na kuvuka barabara ya Morogoro, moja kwa moja aliiendea bajaji iliyokuw imeegeshwa hapo. Hakujua anaelekea wapi, mawazo yote yalikuwa kule alikomuacha Pedeshee, moyo wake ulimsuta, hakujua kama kaua au la.
“Anti mbona husemi tunaelekea wapi?”
“Niache Kimara mwisho” aliropoka wakati hata Kimara yenyewe haijui.
Muda kidogo walifika Kimara. Ashura akashuka na kumpa dereva wa bajaji noti ya elfu tano, hakudai chenji akapotelea mitaani na mkoba wake.
Akiwa ndani ya chumba kidogo, Ashura alijilaza katika kitanda kidogo chenye shuka kuukuu, usingizi haukuja kirahisi, alihisi kama anafuatwa mara kwa mara alishtuka kwa hofu. Alijilaumu kwa nini amechukua begi lile ambalo sasa lilikuwa likimtesa nafsi yake. Ashura hakujua la kufanya, moyoni alimlaumu sana Zai kwa kumdanganya, upande mwingine alimshukuru kwa kuwa sasa kapata pesa za kutosha kufanya lolote. Lakini alijiuliza itakuwaje watakapogundua kuwa yule Pedeshee amekufa mle chumbani, kama jina lake lilikuwa limeandikwa kwenye kitabu cha wageni. Upande mwingine aliona kuwa ni bora Pedeshee afe tu ili asifanye lolote maana kama atapona lazima atamtafuta kwa hali na mali.
Ashura aliuvuta ule mkoba na kumwaga yale maburungutu ya noti kitandani, lo! Hakuamini macho yake, noti nyekundunyekundu nyingi zilizofungwa katika mabunda kwa rubber band yalidondoka kitandani, kwa haraka haraka yalikuwa kama kumi na mbili, alipoingiza mkono ndani ya begi hilo kuona kama yameisha, alihisi anashika kitu cha baridi akakishika kwa kukipapasa akili yake haikugundua ni kitu gani, akakivuta nje, bastola! Ashura alitetemeka na kuitupa chini. Akili ilimzunguka hakujua afanye nini na bunduki hiyo, alibaki ameduwaa na kuishngaa bastola hiyo. Akiwa katikati ya mshangao uliochanganyika na mawazo, alisikia mlango ukigongwa, aliutazama kwa jicho baya na kuanza kusombelea yale maburungutu katika kile kibegi.
€ € € €
Zai alikosa raha, hasa baada ya kuona ukimya mkubwa si kwa Pedeshee wala Ashura, moyoni aliilaumu nafsi yake kuwa bahati kampa Ashura, labda wawili hao wanakula maisha kwenye mji Fulani na hoteli kubwa, kwani alimjua fika Pedeshee kuwa hakutaka shida kwa kitu alichokichagua hasa totos. Lakini haikuwa kawaida ya Pedeshee kuwa kimya, angeshamtumia meseji kusifia kitu alichopata. Hali hii ilimfanya Zai kukosa raha kabisa. Siku hii alichelewa kuamka, alikuta Kautipe ameshaandaa kila kitu mkekani, chain a karimati nne.
“Da Zai, Ashura mpaka saa hizi! Kwani kaenda wapi?” Kautipe alimchokoza Zai kwa swali lililochoma moja kwa moja fikra zake.
“Atarudi tu! Hebu we kunywa chai mi narudi sasa hivi” Zai alimwambia Kautipe, harakaharaka alivaa nguo yake na viatu, akachukua mkoba wake na kuondoka hata alisahau kama hajachana nywele, alikuwa anenda wapi hakujua, ilimradi tu safari. Kila alipompigia pedeshee kwa namba zake zote hakupatikana, jibu lilikuwa lilelile ‘labda jaribu baadae’.
“Mh! Utakuwa ushamuuza mdogo wako!” mmoja wa rafiki zake alimwambia Zai ambaye alionekana kuchanganyikiwa kwa kiasi kikubwa. Maswahiba zake walimpa maneno mengi sana ambayo kwa kiasi Fulani yalimtia kiwewe Zai, hakujua aamue lipi na apuuze lipi. ‘Bora nisingempeleka’ alijiambia moyoni, ‘au niripoti polisi?’ akajiuliza. Aliinua simu yake tena na kuipiga namba ya Pedeshee, jibu lilikuwa ni lilelile tu, hakuna mabadiliko, pepo wa mahangaiko alimkumba, Zai hakujua afanye nini, masaa kwa kwake yalienda mbio sana alitamani baada ya saa sita usiku basi lije saa lingine kabla ya saa saba, saa la ishirini na tano!
€ € € €
Nukushi iliyopo ndani ya ofisi ya Bw. Robinson ilitoa ukulele wa kuashiria kuwa kuna ujumbe wa kupokelewa, Bw. Robinson aliiruhusu na karatasi hiyo kuanza kujiandika polepole, ilipoishia aliivuta na kuitoa pale ilipo na kuanza kuisoma, alikunja sura, na kutabasamu kwa wakati mmoja.
Alipomaliza kazi moja kwa moja alimpitia mkewe kazini kwake na wawili hao wakaelekea nyumbani.
“Darling, nina supraiz nataka kukwambia!”
“Mmmh what beibi?” Bi. Robinson aliuliza kwa kudeka huku akijigeuzageuza kifuani kwa mumewe. Bw. Robinson akaivuta ile karatasi na kumpatia mkewe, mkewe akaisoma kwa makini nakuirudiarudia kana kwamba hakuielewa.
“What?!” aliuliza kwa mshangao mkubwa, akiweka katika kijidroo kilichopo pembeni mwa kitanda chao, akazikusanya nywele zake ndefu na kuzifunga pamoja, kisha akamwangalia usoni mumewe kabla ya kumpiga busu la kimahaba.
“Lini?” akamuuliza mumewe kwa sauti ya upole.
“Wiki ijayo, inabidi tuondoke” Bw. Robinson alimjibu mkewe.
Bw. Robinson alikuwa amepata barua ya kuombwa kubadilisha ofisi ya kazi kutoka Tanzania na kuhamia mahali pengine nje ya Afrika. Kwake halikuwa swala gumu kwani hakuwa na familia, ni yeye na mkewe tu. Walishapita nchi nyingi sana kuishi kwa vipindi tofautitofauti, walihamia Tanzania miezi minne tu iliyopita na sasa wanapata tena uhamisho kuelekea nchi nyingine katika bara jingine.
Mipango ya safari ilifanyika na
kwa kuwa wao walikuwa wakifanya kazi katika ofisi za kibalozi haikuwa shida
kukamilisha mambo yote kwa wakati mfupi.
Walikaa na kufikiri juu ya Tuntufye ‘Jane’, kama wao wanaondoka yeye wamuache vipi na wapi wakati mpaka muda huo hawakuwa hata wanajua wazazi au ndugu zake. Jane alishawaeleza tu kuwa hamjui baba, na hajui mama alipo. Hilo likawa swala gumu kwa wawili hawa, kweli hawakujua wafanye nini, walibaki kuhangaika juu ya hili.
Walikaa na kufikiri juu ya Tuntufye ‘Jane’, kama wao wanaondoka yeye wamuache vipi na wapi wakati mpaka muda huo hawakuwa hata wanajua wazazi au ndugu zake. Jane alishawaeleza tu kuwa hamjui baba, na hajui mama alipo. Hilo likawa swala gumu kwa wawili hawa, kweli hawakujua wafanye nini, walibaki kuhangaika juu ya hili.
6
“Tatizo lenu ubishi
umewajaa!” alizungumza dada wa Mzee Njiku huku akiingia ndani ya gari ya kaka
yake “nilishawaambia, huyu kalogwa hamkutaka kusikia, kiko wapi sasa!”
alimaliza kusema huku akikaa vizuri kitini.
“Lakini maadamu
tumejua hili, tumsake yule mwanamke mchawi kabisa” kaka mtu alisisitiza huku
akiwasha gari na kuingia kwenye barabara hizo za vumbi kurudi mjini.
Walimrudisha kwa nyumba ndogo yake na kumuacha hapo.
Mzee Njiku aliishi
kwa shida sana siku hizo, manyanyaso ya kutoka kwa nyumba ndogo hiyo
yalizidi, wakati mwingine alishinda bila kula ‘nani akupikie! Anayekaa
nyumbani ndio aingie jikoni’, hayo ndiyo yalikuwa majibu.
Usiku mmoja
alisikia kelele za watu wakiongea sebuleni, sauti za kilevi zilipenya masikio
yake, kwa kuwa alikuwa katika lindi la usingizi alijua ni moja ya ndoto za siku
hiyo. Mara alihisi mtu akimsukasuka kumsogeza pembeni.
“Toka! Kakae
sebuleni mwanaume gani wewe, watu tuna mambo yetu” kwa sauti ya kilevi akiwa
anapepesuka huku upande mwingine akikokotana na mwanaume wakiingia chumbani
humo. Nyumba ndogo, alimfukuza chumbani mzee Njiku na kumfukuzia
sebuleni. Mzee Njiku alipepesuka na kujigonga mlangoni baada ya kusukumwa na
mwanaume mwenzake huyo ndani ya nyumba yake, aibu! Alihisi maumivu kichwani
alipojishika alijikuta ana damu mkononi japo si nyingi lakini damu.
Alijikongoja hadi sebuleni huku akiwa na taulo lake kiunoni.
Kutokana na afya
yake kuwa dahaifu sana, Mzee Njiku
aliombwa kustahafu kazi na kuahidiwa kinua mgongo baada ya muda mfupi. Siku
hiyo ilikuwa ngumu kwake, alipompa tarifa hiyo nyumba ndogo wake, ugomvi
mkubwa ulizuka ‘uhame nyumba hii!’ ndiyo kauli iliyosikika mara kwa mara
ndani ya nyumba hiyo. Majirani walipita mbali, hakuna aliyesogea kutoa msaada. ‘Amezidi,
kamuacha mkewe kwa kudanganywa na Kahaba’ mmoja wa wapiti njia
alisema, ‘dawa hizo, kalishwa na kuogeshwa’ mwingine aliongezea. Mzee
Njiku alisukumiziwa nje na kurushiwa kibegi chake ahame. Atafanya nini, alibeba
kibegi chake na kushika suruali yake ili isidondoke, shati lake la Juliana
lilikuwa likipepea kwa upepo, shati ambalo lilikuwa likimkaa vyema mwilini
mwake, sasa lilipepea kana kwamba ndani yake hakukuwa na mwili wa binadamu.
Alisimama mbele ya
nyumba yake aliyokuwa akiishi na na mkewe wa kwanza, mkewe wa ndoa, mwalimu wa
shule ya msingi, aliyemuona hana maana hata, akishirikiana na dada zake hata
kuhakikisha yuko jela miaka mitatu, ukiangalia kisa mapenzi, kapata kitu
kipya, ama kweli kipya kinyemi ingawa kidonda na Mkataa pema pabaya
panamwita.
Machozi yalimtoka,
akiitazama nyumba hiyo kubwa ambayo aliijenga pamoja na mkewe wa ndoa kwa tabu
sana. Sasa ilikuwa mali ya mtu mwingine, alishaiuza na pesa zote kutumbua na
kimada huyo, lo! Mzee Njiku aliketi chini, mchana wa jua kali, waliomjua
walimpita tu na kumwangalia, hakuna msaada amlilie nani.
Breki ya pili ilikuwa kwa kaka yake kumlilia hali, akakaribishwa japo
kwa siku chache ili ajisitiri wakati akitafuta mahali pa kuishi. Ndugu zake
walikutana kujadili yaliyomkuta mwenzao, hasira zikatawala vichwa vyao, chuki
zikajaza nyoyo zao ‘atatutambua mwanamke huyu!,’ mwanamke
aliyependwa na wifi na shemeji zake, leo hii wapendwa hawa wanatamka haya.
Wakaahidi watahakikisha haki inatendeka mpaka nyumba ile ya nyumba ndogo
kwa kuwa ni mali ya kaka yao. Kesi ikapelekwa polisi, jalada likafunguliwa,
mahakama ikachukua mkondo wake, wakati huo Mzee Njiku bado anaegesha kwa
kaka yake.
€ € € €
‘Mh! Polisi au nani?’ Ashura alijiwazia, akafunga vizuri kibegi kile na kuiweka sawia zipu
ya begi lile, akatazama huku na huku hakujua la kufanya, chini pale aliiona
bastola ile ikigaagaa, aliitazama kwa macho yake mawili, hapo akapata picha kumbe
yule jamaa ni jambazi. ‘Zai alikuuza, Zai ni mbaya sana’ upande mmoja wa
roho yake ulimwambia, alishikwa na hasira juu ya Zai, akapata taswira mbaya
kabisa, ‘alitaka iweje?’ Ashura alijiuliza, akashtuliwa na hodi
nyingine, sasa ilikuwa ya nguvu kidogo. Akatzama huku na huku, akaona wazi kuwa
kama ni polisi watamkamata tu, hana la kufanya, akauende mlango taratibu
akachungulia kwenye tundu la ufunguo ‘polisi!’, hakika Ashura alitamani
ardhi ipasuke, alijua sasa mwisho wangu umefika, kujisalimisha utakuwa ujinga
afanye nini, akili ikarudi, alitazama juu ya dali akaona kuna ceilingboard
safi na kajimlango kadogo, kitendo cha haraka aliichukua ile bastola na kuitia
katika kile kibegi, akachomoa noti kiburungutu kimoja na kukificha kwenye taiti
yake aliyoinunua jana jioni baada ya kuacha nguo za ndani kule hotelini,
akasogeza kiti na kukipandisha juu ya kimeza taratibu akweka kile kibegi chake
ndani ya dari na kurudishia kajimlango kale
.
“Karibuni!” Ashura
aliwakaribisha polisi wale wawili, mmoja wa kiume mwenye bunduki na mwingine wa
kike. Yule wa kike akaingia ndani na kumuacha wa kiume mlangoni pamoja na
mhudumu wa guest hiyo, alikiangalia chumba kile kwa macho ya kipolisi,
aliinua godoro na kutazama uvunguni, kasha akaelekea chooni ambako hakukuwa na
kitu zaidi ya sabuni ya kuogea na ndoo, alipekua hapa na pale kisha akaangalia
juu dalini. Ashura ilibaki kidogo mkojo umtoke, alijua sasa siri kubwa
itagundulika, alijikaza kiumwanamke lakini alihisi kama anaishiwa nguvu. Yule
askari akatoka chumbani mle.
“Sio penyewe, hamna
kitu” alimwambia yule wa kiume kasha wakaendelea chumba kinachofuata. Ashura
bila kuchelewa, alitoka hadi kaunta na kukutana na mhudumu wa hapo.
“Dada, nina dharula
naomba kurudisha chumba kama nitarudi nitakujulisha” alilipa chumba na kuondoka
zake, alishuka ngazi haraka haraka, mpaka barabarani, lakini kabla hajaendelea
zaidi kuelekea asikokujua akavutiwa na kundi la watu waliozunguka mbao ya
magazeti. Nae akajipitisha kuona kilichowakusanya ni nini. ‘Jambazi
lililsumbua polisi lanaswa limekufa hotelini’, gazeti moja la kila
siku liliandika habari hiyo na kuweka picha ya mtu huyo, Ashura alipoiona picha
ile ‘rudisha begi langu’ alihisi kama picha hiyo ikimsihi. Akvuta hatua
chache na kupotelea mtaani. Breki ya kwanza ilikuwa ni dukani kwa msambaa
kulikokuwa kukiuzwa kilan aina ya nguo, aliijua aitakayo, baibui nzuri ya
kufunika mwili mzima.
€ € € €
Mama Njiku alichanganyikiwa, hakumuona shoga yake mpaka siku
ya pili, nini kimempata hakujua, kama kafa hakujua, kama anaumwa yuko hospitali
hakujua.
Jua lilizama, kukakucha. Aliwatazama watoto wale wa mama
Vituko ambao usiku wote walikuwa wakimlilia mama yao bila msaada. Mama Njiku
hakuwa na la kufanya, aliichukua simu yake na kumpigia mama Minja wa Manyoni.
“Nimemsubiri sana jana hapa stendi lakini sijamuona” sauti
ya mama Minja ilimkosesha raha mama Njiku ‘kanitoroka,
kaniachia watoto’ , mama Njiku aliangusha machozi huku akiwatazama watoto
wale na wa kwake waliokuwa wakinywa chai asubuhi hiyo, ‘mama atarudi sasa hivi’
aliwafariji, lakini ukweli ni kwamba hakujua nini kimempata shogaye.
“Hapa aliondoka jana asubuhi kuja huko lakini hata sasa hajarudi”
alimueleza mama Minja ambaye nae kwa upande wake alipigwa na butwaa kwa tukio
hilo.
Siku ilikuwa ni ngumu kwa Mama Njiku, kazi haikuweza
kufanyika, kichwa chote kilisambaratika kwa mawazo pa si na majibu.
Mara nyingi alionekana akiegemea mlango kuangalia
labdashigaye huyo atatokea hapa au pale lakini haikuwa hivyo, roho ilimuuma kwa
uchungu masaa yalienda mbio kuliko siku zote, mara jioni ikaifukuza mchana na
usiku ukatawala. Mama Njiku hakusikia hodi wala mlango kusukumwa.
€ € € €
“Umeuza mifugo,
ukatoroka kijijini. Andika maelezo hapa kwenye karatasi hii” polisi mmoja
alimwambia mama Vituko kwa ukali na kumwangalia kwa macho yaliyoonekana
kuchakaa kwa kila namna na gongo.
“Mbona mi
siwaelewi, nani aliyesema mi nimeuza mifugo huko nilikotoka?” Mama Vituko
alijaribu kuwaelza askari wale huku akibubujikwa na machozi.
“Hayo mama utajibia
mahakamani sisi hapa wajibu wetu tumemaliza sawa, haya andika.”
Kwa kauli za askri
yule mama Vituko alielewa kuwa hapo kuna mchezo uliofanyika, alishangaa sana
kuambiwa kuwa eti kosa lake ni kuuza mifugo kasha kutoroka kijijini. Mifugo ya
kwake, mashamba ya kwake, baada ya mumewe kufa ndugu wanataka mali, leo tena
etyi kauza mifugo na kutoroka kijijini, anatafutwa, amepatikana. Mama Vituko alibaki
hana cha kufanya aliumia sana lakini alijuwa wazi kuwa kwa vyovyote ni njama tu
za ndugu wa mumewe baada ya kuona kakataa kurithiwa na kaondoka nyumbani bila
kuaga. ‘Wanataka nini kwangu, masikini mimi? Kila kitu nimewaachia bado tu’,
Mama Vituko alijiwazia moyoni huku akiandika maelezo yote kadiri ya anavyojua.
“We mwanamke! Mbona
umeandika tofauti na maelekezo?” yule askari alimkaripia mama Vituko kisha
akaendelea “sie tumepata oda ya kukutafuta, hivyo kesho utarudishwa kijijini
ulikotoroka ukasomewe kesi yako huko” yule askari alimaliza kuzungumza na
kufunga faili lake kuukuu ambalo lilitimua vumbi kiasi Fulani katika ile meza
yake.
Mama Vituko
alirudishwa selo kusubiri hatima yake ambayo hakuijua ni nini mwishowe.
Aliendelea kusota selo bila kujua lini atatoka. Alikaa ndani mle bila msaada,
hakuna wa kuleta chakula, hakuna kuoga, siku hizo chache zilimfanya abadilike
hata kuonekana kama msukule. Na hii ndiyo hali halisi iliyopo katika
vituo vyetu vya polisi, watu walioonewa na kubambikiwa kesi wanajazwa, polisi
wanawanyima haki zao badala yake unyanyasaji ndiyo unaoshika hatamu.
Baada ya kutoka
katika nondo zile alipokuwa amesimama akiongea jambo na askari mmoja wa kike
Jarina alirudi na kuketi karibu kabisa na mama Vituko.
“Vipi shoga!” mama
Vituko alimuuliza Jarina, msichana waliyekutana naye umohumo selo.
“Mshua anataka
kunitoa, nirudi uraiani” Jarina alimjibu Mama Vituko. Mama Vituko aliposikia
habari hiyo kwake ilikuwa ni furaha sana maana aliona kuwa sasa atapata msaada
kwa namna moja au nyingine. Aliongea naye kwa kirefu na kumpa maagizo Fulani ya
kufanyia kazi akiwa huko uraiani ili kumsaidia, mojawapo lilikuwa ni kuoeleka
taarifa kwa shoga yake Mama Njiku ambaye mpaka muda huo alikuwa hajui lolote.
No comments:
Post a Comment