Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Kairuki, akiongea na wajumbe wa Umoja Wanawake walio katika Sekta ya masuala ya Bahari Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) wakati wa kufunga mkutano wa sita wa mwaka wa umoja huo uliomalizika mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Kairuki (kushoto), akimkabidhi cheti Mkurugenzi Msaidizi kutoka Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Mambo ya Bahari (IMO) Pamela Tansey (kulia) katika hafla ya kufunga mkutano wa sita wa mwaka wa Umoja Wanawake walio katika Sekta ya masuala ya Bahari Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) uliomalizika mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wajumbe mkutano wa sita wa mwaka wa Umoja Wanawake walio katika Sekta ya masuala ya Bahari Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) wakiwa katika mkutano huo uliomalizika mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam.
Wajumbe wa mkutano wa mwaka wa WOMESA wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Ramsmi Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Kairuki (wa tano kutoka kulia waliokaa) ya mara baada ya kufunga wa mkutano huo.
…………………………………………………………………………………………
Na Eleuteri Mangi- MAELEZO
WANAWAKE walio katika Sekta ya masuala ya Bahari wameaswa kupanua wigo wa wanachama walio katika sekta hiyo ili kuongeza ufanisi na tija katika kutekeleza majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Kairuki, alipokuwa akifunga mkutano wa sita wa mwaka wa wa Umoja wanawake walio katika Sekta ya masuala ya Bahari Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) unaomalizika mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam.
Bi. Kairuki alisema kuwa sekta hiyo katika nchi wanachama ni muhimu kulingana na unyeti wake licha ya kukumbwa na changamoto ya kuwa na wataalamu wa kike wachache jambo ambalo WOMESA imelitambua na wanalifanyia kazi kupitia mikutano na semina mbalimbali.
“Ni jukumu lenu WOMESA kushirikiana kwa pamoja ili kuongeza idadi ya wataalamu katika sekta hii mkianzia na wasichana waliopo shuleni na vyuo mbalimbali vya elimu” alisema Bi. Kairuki.
Pamoja na mkutano huo, Bi. Kairuki amewaambia wajumbe hao wa mkutano kuwa anaamini wamepta na kuboresha ujuzi walionao kwa kuwa wameshirikishana na kubadilishana uzoefu kutoka nchi wanachama wa WOMESA ambapo maarifa hayo yataendelea kuwaongezea tija na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao kama akina mama na watalaam katika masuala ya bahari.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa WOMESA kanda ya Afrika kutoka Mauritius Bi. Meenaksi Bhirugnath-Bhookun amesema kuwa WOMESA inakabiliwa na changamoto ya kuwa na wanawake wachache katika sekta ya bahari.
Aidha Bi. Meenaksi amesema kuwa katika mkutano wao wa mwaka wamefikia makubaliano ya kuongeza wanachama kupitia mamlaka za masuala ya bahari, Idara mbalimbali zinazohusu masuala ya bandari, shule za sekondari na vyuo mbalimbali katika nchi wanachama.
Naye Mwenekiti Msaidizi WOMESA tawi la Tanzania Dkt. Tumain Gurumo ambaye pia ni Mhadhiri katika Chuo cha Ubaharia cha Dar es salaam (DMI) amesema kuwa sekta ya bahari inafursa nyingi amewaasa wazazi wawaruhusu watoto wa kike kujiunga kwenye elimu ya bahari ambapo bado kuna fursa nyingi ili waweze kuboresha maisha yao na taifa kwa ujumla.
Dkt. Tumain amewato wasiwasi wazazi na watoto wa kike ambapo amesema kuwa teknolojia imekuwa na imepanua wigo wa wanawake kwenye masuala ya bahari, hivyo wanawake wanaweza kama walivyo wanaume katika sekta hiyo.
katika mkutano huo, WOMESA wamezindua mpango makakati wa miaka mitano unaoanza mwaka 2014 hadi 2019 ikiwa ni mpango wa kuuimarisha umoja huo katika ngazi ya kitaifa na kanda.
Mkutano wa sita wa WOMESA, mwaka huu umeongozwa na kauli mbiu inayosema “Wanawake katika sekta ya bahari baada ya 2014: Wakijenga jukwaa endelevu”.
Nchi zilizoshiriki mkutano huo wa mwaka ni Tanzania, Kenya, Komoro, Mauritius, Namibia na Visiwa vya Shelisheli.
Nchi nyingine ni wanachama ambazo hazikushiriki mkutano wa mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali ni Angola, Sudani, Lesotho, Uganda, Somalia, Eritrea, Botswana, Rwanda, Madagaska, Afrika Kusini, Msumbiji, Burundi, Malawi, Djibout, Zimbabwe, Ethiopia na Zambia.
No comments:
Post a Comment