KATIKA kuhakikisha mkonge unamnufaisha mkulima, serikali imeanza mikakati ya kuendeleza zao hilo.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuongeza uzalishaji wa bidhaa bora zitokanazo na zao hilo kutoka asilimia 2 za sasa hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2015.
Pia kuwepo kwa mbolea za kukuzia zitazosaidia kupata mbegu bora kwa lengo la kupata bidhaa bora itakayoinua kipato cha mkulima na taifa kwa ujumla.
Vilevile serikali itashirikiana na wadau wa sekta hiyo kutoa fursa kwa wananchi wa kawaida kuwekeza zaidi kwenye kilimo na uzalishaji wa bidhaa zitokazo na mkonge.
Kutokana na hali hiyo, Mkurungezi wa Maendeleo ya Katani, Juma Shamte anasema wapo kwenye mazungumzo ya mwisho na kampuni itakayojenga kiwanda kitakachozalisha sukari itakayotokana na mabaki ya mkonge, ambayo itatumiwa na wagonjwa wenye kisukari.
Anataja moja kati ya kampuni zitakazowekeza katika ujenzi wa kiwanda hicho kuwa ni TIERA Group itakayowekeza katika uzalishaji wa sukari kwa kutumia mabaki ya mkonge.
Shamte anasema matokeo ya utafiti uliofanywa na kampuni hiyo, umebaini kwamba mkonge wa Tanzania una sukari nyingi inayoweza kuzalishwa kwa matumizi ya ndani hata kuuza nje ya nchi.
Anasema mazungumzo ya awali yamefanyika kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo itakayofanyika kwa ubia na kampuni za hapa nchini kwa gharama ya dola milioni 10 katika hatua ya awali.
Shamte anasema kiwanda hicho kitakapokamilika ujenzi wake na kuanza kazi, kitawezesha kupungua uhaba wa sukari nchini.
Kwa upande wa mahitaji kwenye soko la dunia, Shamte anasema uhitaji wa bidhaa za mkonge umezidi kuongezeka zaidi ya asilimia 15 ya bei ukilinganisha na mwaka 2000 ambapo bei ilikuwa chini.
Pia ameongeza kuwa serikali itashirikiana na wadau wa sekta hiyo kutoa fursa kwa wazawa kuwekeza zaidi kwenye kilimo pamoja na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na mkonge.
Mkurungenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge, Hamisi Mapinda, anasema mwaka 2013 sekta hiyo ilizalisha zaidi ya tani 35,589 za singa na kushika nafasi ya pili kwa uzalishaji wa mkonge duniani.
Anasema katika mwaka 2012 waliuza nje ya nchi tani 15,541 za singa na kufanikiwa kupata sh bilioni 21.1 ikilinganishwa na tani 11,670 zilizouzwa ndani ya nchi na kupata sh bilioni 17.7.
Mapinda anasema bodi kwa kushirikiana na wazalishaji wa mkonge nchini inatekeleza mpango wa maendeleo ya sekta hiyo wa mwaka 2012 hadi 2021 unaolenga kuongeza matumizi ya mmea wa mkonge.
Mkurungezi Mtendaji wa Kampuni ya Katani Limited, Salum Shamte, anasema endapo wadau wa maendeleo wakiwemo viongozi na wananchi watakuwa tayari kushirikiana kwa dhati, kuna uwezekano mkubwa Mkoa wa Tanga kurejea kwenye hali bora ya uchumi kama wa zamani.
Anasema ili Tanga iweze kupiga hatua kiuchumi, sekta binafsi na zile za umma hazina budi kujadiliana mambo mbalimbali jambo litakalosaidia kuwezesha shughuli za kiuchumi kama kilimo cha mkonge kuimarika.
Mkurugenzi huyo anasema kampuni yake imekuwa ikisukuma mbele mfumo wa kilimo cha wakulima wadogo wadogo ingawaje pia wamekuwa wakiwaunga mkono wakulima wa kati na wakubwa lengo likiwa kuimarisha kilimo hicho ili uchumi kukua.
“Sisi Kampuni ya Katani tunasukuma kilimo cha wakulima wadogo wadogo, hatusemi kilimo hicho ndiyo kitainua uchumi pekee bali hata wakulima wa kati na wakubwa wote tuko tayari kuwaunga mkono kwani kama wote tutashirikiana kwa dhati, Tanga itarejea hali yake ya kiuchumi,” anasema.
Akizungumzia manufaa ya kilimo cha mkonge, anasema kinamwezesha mkulima kuhudumia zaidi ya zao moja kwenye eneo moja ambapo pia kwa nguvu kazi ile ile wanaweza kuzalisha mkonge na mazao mengine ya chakula. Katika hilo anasisitiza kwamba kilimo hicho kina tija.
Anabaisha kwamba kwa sasa kuna wakulima 2,150 waliojiunga na mfumo wa kilimo cha wakulima wadogo unaofahamika kama SISO kwenye mashamba matano ya katani tangu Desemba 2011; asilimia 14 ni wanawake.
Anasema kampuni inatoa huduma mbalimbali kwa wakulima zikiwemo zile za ugani, taaluma ya ufundi, kusindika mkonge, kutafuta masoko ya singa na bidhaa zinazotokana na mkonge, kuwaunganisha na kuwapa elimu ya biashara ili kilimo hicho kiwe na faida.
Mambo mengine ni usimamizi wa mpango, huduma ya utayarishaji wa ardhi kwa kulima na kupanda na kufanya utafiti ili kuongeza matumizi ya mkonge, kuwawezesha kuboresha kipato chao na kuwahamasisha wakulima kujiunga katika vikundi na vyama vya ushirika.
Kuhusu maendeleo ya utekelezaji kwenye mikoa mingine nchini, anasema mfumo wa SISO umeanza kuhamasisha kilimo cha mkonge kitaalamu na kibiashara katika Wilaya ya Kishapu, Shinyanga.
Anasema Katani kwa kushirikiana na Shirika la Oxfam na Bodi ya mkonge wameanzisha kilimo cha mkonge chenye kulenga wakulima 16,500 kwenye vijiji mbalimbali.
Mwenyekiti wa Wakulima Wadogo, Frederick Malika, anasema changamoto zinazowakabili katika uzalishaji wa zao hilo ni mvutano wa bei uliopo na ugawaji wa pato kati ya mwekezaji na mkulima pamoja na mwekezaji mwenye viwanda vya kusindika mkonge.
“Mpaka sasa hatujajua bei sahihi ya kuuzia zao hili tunalopaswa kutozwa kama wakulima wadogo kwani gharama ya kukuza mkonge mdogo ni kubwa kwa mkulima ukilinganisha na kipato anachokipata,” anasema Malika.
Pia anasema kama kiwanda hicho cha kuzalisha sukari kitajengwa nchini itasaidia wakulima wa zao hilo kuwa na soko la uhakika pamoja na kumfaidisha mkulima wa zao hilo.
Anasema eneo jingine linalohitaji msukumo zaidi ni la ufufuaji wa mkonge baada ya bei ya zao hilo kupanda katika soko la dunia.
No comments:
Post a Comment