Kigamboni wamkaba koo Waziri Tibaijuka
Na Nuzulack Dausen, Mwananchi
Posted Jumatatu,Agosti11 2014 saa 10:53 AM
Posted Jumatatu,Agosti11 2014 saa 10:53 AM
Kwa ufupi
Pamoja na wito huo, viongozi hao walitaka mpango wa
Serikali wa kuwataka wananchi kununua hisa za uendelezaji mji huo kwa
asilimia 10 ya malipo ya fidia, uwe wa hiari na Serikali isiingilie
uamuzi huo.
Dar es Salaam. Viongozi wa Mji wa Kigamboni
wamemtaka Waziri wa Ardhi na Maendeleo na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
kuharakisha malipo ya fidia kwa wakazi watakaopisha ujenzi wa mji mpya
na kuacha mikutano ya hadhara isiyokuwa na tija.
Pamoja na wito huo, viongozi hao walitaka mpango
wa Serikali wa kuwataka wananchi kununua hisa za uendelezaji mji huo kwa
asilimia 10 ya malipo ya fidia, uwe wa hiari na Serikali isiingilie
uamuzi huo.
Wakizungumza jana katika semina maalumu kati ya
Prof Tibaijuka na viongozi wa mji huo, viongozi hao walisema wakazi wao
wamechoka kucheleweshewa malipo yao na kwamba hakuna mkutano wa hadhara
utakaofanyika kabla ya masilahi kutimizwa.
Diwani wa Kata ya Kibada, Juma Nkumbi alisema
tatizo la uendelezaji mji huo lipo wizarani na si kwa wananchi, kwani
wakazi wa maeneo ya Kibada na Uvumba walishakubali kupisha ujenzi huo.
“Asilimia 90 ya wakazi Uvumba na Kibada wako
tayari na walishafanyiwa tathmini na kupata mrejesho wa fidia zao,
lakini sasa ni mwaka na miezi sita hakuna aliyelipwa,” alisema Nkumbi na
kuongeza:
“Natoa tahadhari... kusubiri sana bila mafanikio ni hatari.”
Awali, katika semina hiyo Prof Tibaijuka aliwasihi
viongozi hao kuwaeleza wananchi wao umuhimu wa kununua hisa za taasisi
itakayowekeza uendelezaji wa mji huo ili wawe sehemu ya wamiliki.
Alisema kuwa hatapenda kuona wakazi wa eneo hilo
wakihama mji na kushuhudia watu wa nje wakinufaika na eneo hilo
aliloliita “dhahabu” ya miaka ijayo.
“Itapendeza kama wananchi watakubali kukatwa
asilimia 10 ya sehemu ya fidia yao ili iwe malipo ya hisa za kumiliki
mji huu. Nitaonekana nimeshindwa, iwapo wananchi watachukua fidia na
kuondoka kwenye ardhi ambayo itakuwa dhahabu,” alisema Prof Tibaijuka.
Hata hivyo, Mbunge wa Kigamboni Faustine
Ndungulile alisema suala la hisa liwe hiari na serikali iweke bayana ni
taasisi ipi na namna gani itawekeza fedha hizo ili iwapatie faida wakazi
hao.
“Waziri naomba uwajibu wananchi masuala hayo na
kama hautaweza mimi sitakuunga mkono hata kidogo. Ni lazima wananchi
2800 wanaosubiri fidia zao wayajue haya,” alisema.
Ndungulile alionekana kutoridhishwa na sehemu
kubwa ya utekelezaji wa mradi wa mji mpya alisema wananchi hao wamechoka
na maneno matupu ya serikali bila ya kuwa na fedha za kutosha
No comments:
Post a Comment