Watangazaji Kibonde, Gadna watiwa mbaroni
Na Thommy kundy, Mwananchi
Posted Jumanne,Agosti12 2014 saa 14:30 PM
Posted Jumanne,Agosti12 2014 saa 14:30 PM
Kwa ufupi
Taarifa zinadai watangazaji hao hawakuwa katika hali ya kawaida kutokana na lugha chafu walizokuwa wakitoa kwa polisi.
Watangazaji wawili wa Clouds FM, Ephrahim
Kibonde na Gadna Habash wamekamatwa na polisi kwa madai ya kusababisha
ajali na kutoa lugha ya matusi kwa polisi.
Kibonde na Gadna wanadaiwa kusababisha ajali hiyo jana katika eneo la Makumbusho, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kibonde ndiye alikuwa dereva wa gari linalodaiwa
kusababisha ajali hiyo kwa kugonga gari la raia wa kigeni na kukimbia
wakati askari wa usalama barabarani (trafiki) walipofika kupima ajali
hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni,
Camilius Wambura alithibitisha kukamatwa kwa watangazaji hao, “Ni kweli
tunawashikilia watangazaji hao kwa kosa la kukaidi amri ya polisi, bado
tunawashikilia mpaka sasa.”
Ilidaiwa kuwa gari la Kibonde iligonga gari hilo
kwa nyuma na trafiki walipofika ili kupima alikimbia, ndipo trafiki
walipotumia gari lililogongwa kumfukuzia na kufanikiwa kumkamata.
Akisimulia kisa hicho polisi wa kike katika Kituo
cha Oysterbay ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema Kibonde
alikataa kutii sheria bila shuruti kwa kivuli cha umaarufu alionao.
“Hawa wanashikiliwa kwa kosa la kuvunja sheria za
barabarani, Kibonde alikuwa anaendesha akiwa amelewa na kusababisha
ajali, kama haitoshi walikimbia na kuwatolea polisi lugha chafu za
matusi jambo ambalo ni kinyume na sheria,” alisema askari huyo.
Alisema walipoanza kuwafukuzia waliwakamata Kituo
cha Mwenge na trafiki aliingia katika gari lake na kumwomba arudi eneo
la ajali ili wakapime ajali. Kibonde aligoma na kumtaka trafiki ashuke
katika gari lake, trafiki naye akagoma kushuka.
“Kibonde alikaidi tena na kuondoa gari na
kuendelea na safari yake wakati trafiki akiwa ndani ya gari hiyo,
aliwasiliana na wenzake ambao walianza kuifuatilia gari hiyo, walipofika
eneo la Ubungo mataa, trafiki mwingine aliisimamisha gari na Kibonde
alikaidi kusimama, akiwa katika hali hiyo kuna gari ilitokea ikakatisha
kati ya trafiki na gari hiyo ndiyo kikawa kigingi cha gari ya Kibonde na
kutiwa mbaroni,” alisema polisi huyo.
Baada ya kukamatwa, Kibonde na abiria wake
walifikishwa katika Kituo cha Polisi Urafiki Ubungo saa 7:00 asubuhi na
baadaye saa 8:00 asubuhi walihamishiwa katika Kituo cha Oysterbay.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Osterbay, Victor Samata
aliliambia gazeti hili kuwa suala hilo lipo juu ya uwezo wake
kulizungumzia kwani yeye siyo msemaji, hivyo kumtaka mwandishi amtafute
msemaji wa kituo hicho.
“Sidhani kama hili ni suala la kulijadili,
isitoshe mimi siyo msemaji wa hapa ingefaa atafutwe msemaji
kulizungumzia hili,” alisema Samata.
No comments:
Post a Comment