Blogger Widgets FURSA KWA VIJANA WOTE TUPAMBANE KWA KILA NJIA ILI MRADI TUWEZE KUEPUKA HUU UMASKINI TANZANI NA AMIN KILA ATAFUTAYE KWA NIA HUPATA MAANA ATA MAANDIKO HUSEMA PENYE NIA PANA NJIA

Monday, September 29, 2014

‘Katiba itaibeba CCM Zanzibar’



Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ),
Mohamed Aboud Mohamed amesema Katiba inayopendekezwa, itaibeba CCM katika 
uchaguzi mkuu ujao visiwani humo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu bungeni jana, Aboud alisema katiba hiyo 
 itawasaidia katika kujibu kero mbalimbali zilizokuwa zikitolewa kwani imejibu 
asilimia 90 ya kero hizo.
"Kwa asilimia zaidi ya 90 kero za muda mrefu za wananchi wa Zanzibar zimejibiwa. 
Kwa hiyo wananchi watajua kuwa tumeshughulika na kero zao kwa kuzipatia 
ufumbuzi,"alisema.
Aboud alisema watakwenda kwa wananchi wa Zanzibar wakiwa kifua mbele 
kufafanulia kero ambazo zimetafutiwa ufumbuzi na wajumbe wa Bunge la 
Katiba, wengi wao wakitokana na CCM.
"Mimi ninaamini kuwa wananchi wakipelekewa Rasimu ya Katiba hii 
 inayopendekezwa na wakaiona kuwa imekidhi matakwa yao wataiunga 
mkono,"alisema Aboud katika mahojiano hayo.
Aeleza kuhusu urais 2015 (t.k)
Waziri huyo ambaye aliwahi kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar mara mbili 
 (mwaka 2000 baada ya Dk Salmin Amour kumaliza muda wake na mwaka 2010 
 wakati Amani Abeid Karume alipokuwa akiondoka madarakani), alisema 
 hatagombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015.
"Sina nia wala dhamira ya kugombea tena urais. Mimi dhamira yangu kubwa 
ilikuwa ni kuiunganisha Zanzibar kazi ambayo Rais aliopo (Dk Ali Mohamed Shein) 
ameifanya vizuri,"alisema.
Aboud alisema sifa ya Rais ni uadilifu na kuwaunganisha Wazanzibari na 
Watanzania kwa jumla, sifa ambazo zote amekuwa nazo Rais wa Serikali ya 
 Mapinduzi ya Zanzibar Dk Shein. Hata hivyo, alisema kazi yoyote 
inayofanywa na mwanadamu inakuwa na upungufu, haiwezi kuwa kamili.
"Mimi nina uhakika matarajio ya Wazanzibari yamepata majibu katika 
Rasimu hii ya Katiba. Na ninaamini kuwa wataipokea vizuri. Lazima 
tufahamu kuwa Katiba ni mchakato," alisema.
Aboud alisema kama kuna jambo ambalo hawakulipata katika mchakato 
wa sasa wa Katiba unaomalizika Oktoba 4 au hawakufikia mwafaka , 
kesho wanaweza kupata nafasi ya kulizungumza.
Alipoulizwa kero zilizopatiwa ufumbuzi katika Katiba hiyo, Aboud aliitaja 
kero ya mafuta na gesi ambapo sasa Zanzibar itakuwa na uwezo wa kushughulikia.
"Zanzibar sasa itaweza kutunga sheria na sera zake za kushughulikia mafuta 
na gesi, lingine lilikuwa ni ushiriki wa Zanzibar katika taasisi za 
kimataifa," alisema Aboud.
Alisema Rasimu imetoa haki ya Zanzibar katika mikopo na imetoa fursa ya 
kupunguzwa kwa mambo ya muungano ambayo ilikuwa ni sehemu ya kero 
ya Wazanzibari.
Ukawa kuondoka bungeni
Aboud alisema Ukawa na wajumbe wanaotokana na CUF, kususia Bunge hilo, 
hiyo haitaathiri uendeshaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa vile bado 
wana umoja.
"Hawa walijitoa si kwa sababu hawaoni umuhimu wa Bunge la Katiba. 
Walijitoa kwa sababu waliamini suala la serikali tatu ni suala la msingi. 
Sisi tumeona mfumo wa Serikali mbili ndiyo utakaodumisha muungano," 
alisema na kuongeza:
"Sisi tumejali sana masilahi ya wananchi, sasa wao pengine wamejali sana 
masilahi yao. Sisi tumeona kuwa mfumo wa serikali mbili ndiyo utaweka 
msingi wa muungano."
Alisema pengine CUF wamejali sana faida watakazopata kutokana na mfumo 
wa serikali tatu.
"Wanajua wao kwa nini wanataka mfumo wa Serikali tatu. Lakini kwa mimi na
 imani kabisa serikali mbili ndiyo njia sahihi," alisema Aboud.

No comments:

Post a Comment

TUPAMBANE BLOG