Na Thommy kundy, MAELEZO
Askari wa
Jeshi la Zimamoto na uokoaji nchini wametakiwa kuwa waadilifu,
waaminifu, watii na watekelezaji wa sheria zote za nchi kwa kuwa hizo ni
miongoni mwa sifa za askari bora.
Akifunga
rasmi mafunzo ya awali ya uzimaji wa moto katika viwanja vya ndege kwa
askari 100 wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji katika kambi ya Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Airwing, Ukonga jijini Dar es salaam, Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Pereira Ame Silima amewataka
askari hao kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani vitawapelekea
kufukuzwa kazi na kukatisha ndoto za maisha yao.
Alisema
nidhamu ya kazi, Ushirikiano na kujituma katika mema ni miongoni mwa
mambo matatu yatakayowasaidia askari hao kufanikiwa katika kazi zao
pamoja na maisha yao kwa ujumla.(Victor Simon)
Naibu
waziri huyo aliwahakikishia askari hao kuwa Serikali itaboresha
miundombinu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ikiwa ni pamoja na kuwapatia
vitendea kazi vya kisasa ikiwemo mitambo ya kisasa ya uzimaji wa moto
na uokoaji na vyuo vya mafunzo ili jeshi hilo liondokane na changamoto
zilizopo kwa haraka.
Akizungumza
awali, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Viwanja vya ndege Mhandisi Thomas
Haule aliiomba serikali kuimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa
kuwapatia vifaa vya mafunzo vya kisasa pamoja na mafunzo ili kuendeleza
huduma bora zinazotolewa na viwanja vya ndege nchini.
Alisema
teknolojia ya kisasa na hasa magari ya zimamoto ya kisasa yanahitajika
ili kupanua viwanja vya ndege nchini. Hivi sasa kuna kituo kimoja cha
zimamoto katika kiwanja cha ndege cha Dar es salaam na baada ya
kukamilika kwa ujenzi wa Sehemu ya tatu (Terminal 3) ya uwanja huo
kitahitajika kituo kingine ikiwa ni pamoja na kupanda hadhi kwa kiwanja
hicho kutoka category 9 hadi ya 10.
Wakati
huo huo, Kaimu Kamishna Generali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Lt. Col
Lidwino Simon Mgumba alisema lengo la mafunzo hayo kwa askari wa
Zimamoto na Uokoaji ni kukabiliana na upungufu wa askari katika vituo
vilivyoko kwenye viwanja vya ndege. Aliongeza kuwa mafunzo hayo yalianza
na askari 101 na kumalizika na askari 100 ambapo askari mmoja alitoroka
mafunzo baada ya kushindwa kuhimili mafunzo hayo.
Aidha
kabla ya kufunga mafunzo hayo, Mgeni rasmi alishuhudia onyesho la
uzimaji wa moto kwenye ndege iliyowaka likifuatiwa na gwaride ambalo
alilikagua na baadaye kulifuatiwa na kiapo cha utii kwa askari waliofuzu
mafunzo hayo
Mafunzo
hayo ya miezi miwili ya uzimaji wa moto kwenye viwanja vya ndege kwa
askari wa jeshi la Zimamoto na uokoaji yamefanyika katika awamu ya pili
ambapo awamu ya kwanza yalifanyika mwaka jana.
No comments:
Post a Comment