Blogger Widgets FURSA KWA VIJANA WOTE TUPAMBANE KWA KILA NJIA ILI MRADI TUWEZE KUEPUKA HUU UMASKINI TANZANI NA AMIN KILA ATAFUTAYE KWA NIA HUPATA MAANA ATA MAANDIKO HUSEMA PENYE NIA PANA NJIA

Friday, October 17, 2014

JINI ALINIOKOA NISIBAKWE NA SANGOMA-5

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Stumai alipokuwa akipiga kelele na kumuonyesha baba yake jini aliyejigawa mara mbili alipotaka kumchukua  lakini mzazi wake hakumuona badala yake alimuona paka mweusi. Binti yake alimwambia hakuwa paka bali ni yule jini. Je, kilifuatia nini? Songa mbele..
Baba alichukua fimbo akawa anamfukuza yule paka lakini hakukimbia, baadaye alifungua mlango kwa kutumia ile fimbo akampiga kichwani papo hapo akalalamika kwa kusema;
“Jamani mkono wangu!”
Nilipomuuliza mkono ulifanyaje akawa anaendelea kulalamika kwa maumivu aliyopata ndipo mama aliamka, jambo la kushangaza muda uleule mkono wake ulivimba sana.Mama alipomuuliza alipatwa na masaibu gani, alimwelezea ndipo akashauri waende hospitali lakini baba aligoma na kumwambia tatizo lake halikuwa la hospitali bali la kiswahili.
Kufuatia baba kulalamika kwa maumivu, mama alichukua dawa ya kuchua akamchua lakini hakupata nafuu ndipo alisema tulale kukicha angejua cha kufanya.Wakati huo, yule mtu alikuwa ameondoka ndipo tulikaa pale sebuleni tukimwangalia baba aliyekuwa akilalamika kwa maumivu hadi kulipokucha.
Kutokana  tatizo la baba kutokea katika mazingira ya kutatanisha, mama alimuuliza kama alikuwa anamfahamu shehe yeyote ili wakamweleze awasaidie.Baba alisema alikuwepo lakini alishauri kwa wakati ule tusubiri kwanza ajitazamie hali yake, mama alichemsha maji ya moto akamchua baba, hata hivyo uvimbe haukupungua.
Tukiwa tumekaa, baba alimtuma mdogo wangu Said aende kutoa taarifa kwa ndugu zake waliokuwa wakiishi Temeke Mikoroshini kwamba mimi nilikuwa nina matatizo.Mdogo wangu huyo alikwenda, baada ya kupewa taarifa hiyo mama yangu mdogo alikuja akaelezwa matatizo yangu mpaka baba alivyovimba mkono kufuatia kumpiga paka.
Baba alimweleza kwa kuwa yeye alikuwa mgonjwa, siku iliyofuata aende akanichukulie uhamisho shuleni ili nihamie Shule ya Msingi Temeke.Mama yangu huyo alikubali kufanya kazi hiyo siku ya Jumatatu, baada ya maongezi mama mdogo aliondoka na kuelekea Temeke Mikoroshini alikokuwa akiishi.
Kufuatia baba kutopata nafuu, mama alimshauri waende hospitali lakini alipinga na kumwambia kama kulikuwa na mtaalam wa dawa za jadi aliyemfahamu afuatwe kwa sababu ugonjwa wake haukuwa wa hospitali.Saa kumi na moja jioni, mama alimtuma mdogo wangu akamwite mtaalam huyo ambaye alifika saa kumi na mbili, akasimuliwa kisa changu chote na mkasa uliompata baba.
Mganga huyo alisema nilipatwa na tatizo kubwa sana ambalo kulitatua ingekuwa gharama kubwa, alimuuliza baba kama angeziweza gharama hizo.Kwa kuwa hakuwa na fedha aliahidi kuuza kitu chochote ili apate pesa za kuniondolea tatizo lililokuwa likinikabili, yule mganga akasema sawa.
Kwa vile alikuja na baadhi ya dawa, akaziandaa na kumpaka baba mkononi na nyingine alimwambia mama akaniogeshe kisha mabaki yatakayoanguka chini ayaokote na kuyaweka kwenye chombo.
Aliongeza kuwa, baada ya kufanya hivyo mimi na mganga tungeenda kuyamwaga yale mabaki ya dawa jalalani ikiwa ni kuanza tiba ya tatizo langu.
Mama aliuliza kazi hiyo ingefanyika saa ngapi, akamwambia ni muda uleule yaani kabla jua alijazama, mama akauliza si watu wangetuona, akamwambia tungetumia ujanja ili  wasitushtukie.Kama alivyosema, tuliondoka mimi, mganga ambapo mama alitufuata kwa nyuma hadi kwenye jalala ambalo lilikuwa nyuma ya nyumba tuliyokuwa tukiishi.
Tulipofika pale watu wakawa wanapita ndipo ‘tulijibalaguza’ kama vile tunazungumza, mganga akamwambia mama atusubiri, mimi na yeye tukasogea hadi kweli lile jalala.Kabla hatujamwaga ile dawa, nikahisi baridi na mwili kunisisimka, nikajua yule mtu wangu angenitokea, nikamwuliza mganga kama mtu aliyekuwa akitokea ataibuka pale angefanyaje?
Mtaalam huyo alinitoa wasiwasi kwamba asingeweza kunitokea akaniambia tusogee kwenye lile shimo la taka, tuliposogea nilipotupa macho yangu mbele nililiona bonge la joka lina rangi mchanganyiko likituangalia huku limeinua kichwa.
Kitendo cha kuliona joka hilo moyo ulipiga paa, nikamwambia yule mganga kwamba mtu aliyekuwa akinitokea alikuja kwa staili nyingine.Mganga aliniuliza staili gani? Nikamwambia ya nyoka na kumwambia aangalie pale kwenye jalala lakini alipoangalia hakumuona.
Yule mganga aliniuliza mbona hakuona kitu nikasisitiza aangalie vizuri ndipo yule mganga akashtuka na kusema aliliona lile joka.Jambo la kushangaza lile joka likawa linajikunja na kujikunjua na kuinua kichwa chake bila kutufuata, yule babu mganga akasema kama mambo yenyewe yalikuwa vile asingeweza kunitibia.
“Haya mambo makubwa sana, kazi yako nimeshindwa mtafuteni mganga mwingine,” Stumai alimkariri yule mganga.Baada ya mganga kutoa kauli hiyo nilimwuliza  kama yeye niliyemtegemea angenitibia alisema vile ingekuwaje kwa upande wangu? Akasema mambo yangu yalikuwa makubwa asingeyaweza.

No comments:

Post a Comment

TUPAMBANE BLOG