Blogger Widgets FURSA KWA VIJANA WOTE TUPAMBANE KWA KILA NJIA ILI MRADI TUWEZE KUEPUKA HUU UMASKINI TANZANI NA AMIN KILA ATAFUTAYE KWA NIA HUPATA MAANA ATA MAANDIKO HUSEMA PENYE NIA PANA NJIA

Wednesday, October 15, 2014

Kwanini Julius Nyerere Alitoa Machozi Hadharani Tabora?

  • Written by Tupambane Blog
  • Share on facebook Share on gmail Share on twitter 
Ndugu zangu,
Katika Siku hii ya Mwalimu, nitarejea hapa moja ya mazungumzo muhimu ya kihistoria niliyopata bahati ya kuyafanya; ilikuwa ni jioni ya Januari 24, 2012 pale nilipokutana na Mama Mosi Tambwe ( sasa marehemu) nyumbani kwake Tabora Mjini.
Mosi Tambwe aliingia TANU akiwa na miaka 18. Ni mmoja wa wanawake mahiri sana kisiasa wa enzi hizo. Mosi Tambwe alinisimulia, kuwa alianzia kwenye TANU Bantu Group, hiki kilikuwa ni kikundi cha vijana ndani ya TANU, ambacho baadaye kikawa TANU Youth League.
Kwa kirefu kabisa Mosi Tambwe aliniambia majukumu yao kama vijana kwa wakati huo. Ni wakati nchi ikiwa chini ya mkoloni. Akanielezea pia majukumu hayo yalivyobadilika baada ya uhuru. Enzi hizo vijana walikuwa wakiandaliwa kupitia TANU Youth League ili waje kuwa makada wa chama, hivyo basi, viongozi wa wananchi walinolewa vema. Walijengewa uwezo wa kujenga hoja.
Ni enzi hizo, baada ya kutoka Chipukizi, hatua iliyofuata ni Tanu Youth League. Wengine wakaenda JKT na hata Jeshini. Azma kubwa ilikuwa kujenga Uzalendo na Umoja wa Kitaifa.
Kwanini Julius Nyerere alitokwa na machozi mkutanoni pale Tabora? Nilimwuliza Mosi Tambwe.
- Unajua, siku ile Mwalimu alisimama akiongea, na mbele yake kulikuwa na Kituo Cha Polisi. Juu kwenye paa ya jengo hilo alisimama askari wa kikoloni aliyekuwa akiufuatilia mkutano huo akiwa na silaha mkononi. Jambo lile lilimtia huzuni sana Mwalimu, alijikuta akitoa machozi. Aliniambia Mama Mosi Tambwe ( Pichani)(T.K)
Na unapomsikiliza Mama Mosi Tambwe unaiona tofauti kubwa ya vijana wa wakati huo na wa sasa.
Tumekosea wapi?
Jibu; ni pale, kwa shinikizo la mabadiliko ya dunia , na kwa shingo upande, chama tawala kiliporidhia kurejesha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. CCM ikasahau kuratibu mabadiliko makubwa ya kikatiba ambayo yalipaswa yaendane na mabadiliko hayo ya kimfumo.
Kimsingi, hali tuliyo nayo sasa ya kuchanganyikiwa, hata kwenye hili la vyama kuunda vikosi vya ulinzi badala vya kiitikadi. Hii inatokana na makosa makubwa, kama Taifa, tuliyoyafanya mwaka 1992.
Nimeandika mara kadhaa, kuwa historia ni mwalimu mzuri, lakini, wakati ni mwalimu mzuri pia. Tujifunze kutokana na mabadiliko ya wakati. Katika wakati tulio nao sasa, vyama vya siasa havipaswi kujiundia vikundi vya ulinzi vyenye kupata hata mafunzo ya kijeshi. Ni ujasiri, kama viongozi wa sasa watazipa mgongo fikra hizi za kizamani na kuendana na mabadiliko ya wakati.
Tufanye nini?
Kama ningeombwa ushauri hii leo, basi, ningevishauri vyama vya siasa, kuwa kwa haraka sana, viachane na harakati za kuunda vikosi au vikundi vya ulinzi. Jukumu hilo liachiwe vyombo vya usalama, hususan Jeshi la Polisi, na hata makampuni ya ulinzi yenye kutambulika kisheria.
Na vile vilivyopo vivunjwe. Maana, vikundi hivi vya ulinzi ambavyo kimsingi ni vikundi vya wanamgambo wa vyama ni maafa tunayoyaandaa wenyewe. Kama hatutanguliza busara na hekima, basi, itakuwa ni suala la wakati tu kabla hatujajikuta kwenye dimbwi la maafa makubwa. Tumeshaziona ishara.
Kwa vyama vya siasa, badala ya kutumia muda na rasilimali zao kufyeka mapori ya kuwaweka vijana kwenye ' makambi ya ukakamavu', umefika wakati sasa wa kubadilika, kuachana na fikra hizo za kijima zenye kuturudisha nyuma miaka 50.
Huu ni wakati wa kuwajengea vijana wa vyama ' ukakamavu wa akili'.
Zimepita, zama za ' Umkhoto we Sizwe'. Hizi ni zama za ' Umkhoto we Mitwe'- Ni mapambano ya kutumia vichwa kwa maana ya akili.
Naam, ukiona zinduna na ambali iko nyuma.

No comments:

Post a Comment

TUPAMBANE BLOG