Blogger Widgets FURSA KWA VIJANA WOTE TUPAMBANE KWA KILA NJIA ILI MRADI TUWEZE KUEPUKA HUU UMASKINI TANZANI NA AMIN KILA ATAFUTAYE KWA NIA HUPATA MAANA ATA MAANDIKO HUSEMA PENYE NIA PANA NJIA

Monday, November 17, 2014

ACHENI KUWABEMBELEZA WAWEKEZAJI WASIOZINGATIA SHERIA ZA MAZINGIRA- KAIMU KATIBU TAWALA MBEYA


Picha Na 3 (1)
Na Greyson Mwase, Mbeya
Maafisa Mazingira katika   wilaya zilizopo katika mikoa ya Iringa na Mbeya wametakiwa kuacha kuwabembeleza wawekezaji wasiozingatia sheria za uhifadhi wa mazingira.
Kauli hiyo imetolewa na  Kaimu Katibu  Tawala Mkoa wa Mbeya , Constantine Mushi wakati akifungua mafunzo  ya siku  tano yaliyoshirikisha maafisa mazingira kutoka katika wilaya  14 za mikoa ya Iringa na Mbeya ikiwa ni pamoja na  Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)  na Ofisi ya  Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mushi alisema kuwa   wapo baadhi ya wawekezaji katika sekta za madini na nishati wasiozingatia sheria ya mazingira ya mwaka 2004 inayotaka shughuli yoyote ya maendeleo  kuendana na uhifadhi wa mazingira na hivyo kuchangia uharibifu mkubwa wa mazingira.
Alisema kuwa maafisa mazingira wanatakiwa kusimamia  sheria za mazingira kwa kuhakikisha kuwa zinafuatwa ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kali wawekezaji wasiozingatia sheria hizo.
Alisema kuwa katika sekta ya nishati kuna shughuli za utafutaji  wa mafuta na gesi unaoendelea sehemu mbalimbali nchini  katika  nchi kavu, kwenye  ukanda wa bahari, katika maji ya kina kirefu baharini (deep sea) na kwenye maziwa na kusisitiza kuwa hii ni  changamoto kwa maafisa mazingira katika kutoa ushauri na kuhakikisha kuwa binadamu  na viumbe wengine hai hawaathiriwi na uwekezaji huu.
Alieleza kuwa uwekezaji katika sekta ya nishati ni mkubwa sana kwani nishati ya umeme ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo suala la mazingira linatakiwa lizingatiwe ili kuhakikisha kuwa wananchi na  viumbe wengine hawaathiriwi na uwekezaji huu.
Aliongeza kuwa uwekezaji katika sekta ya madini  katika miaka ya karibuni  umekua kwa kasi kubwa sana lengo lake likiwa ni kuleta maendeleo na kusisitiza kuwa shughuli za uchimbaji madini zisipofuata kanuni na  sheria za mazingira zinaweza kuacha nchi ikiwa jangwa na kuathiri mabadiliko ya tabia nchi.
“Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa shughuli zote za maendeleo zinafanyika bila kuleta athari kubwa katika mazingira yetu kwa kusimamia sheria na kanuni za mazingira pasipokuwa na upendeleo,” alisisitiza Mushi.
Alisema kuwa kuzingatia hitaji  la sheria ya mazingira, Wizara ya Nishati na Madini  imeandaa mpango kazi wa mazingira wa sekta za nishati na madini (sector environmental action plan) ambao utekelezaji wake utaenda hadi katika ngazi ya wilaya.
Wakati huo huo Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, Wizara  ya Nishati na Madini Mhandisi Gideon Kasege alisema lengo la mafunzo hayo  ni kuwashirikisha  maafisa mazingira mpango kazi wa mazingira  wa sekta za nishati na madini  wa Wizara,  kuwapa elimu ya mazingira  na kupata michango yao ili kuwa na mkakati wa pamoja wa kuhakikisha kuwa sheria na kanuni za mazingira zinafuatwa.
Mhandisi Kasege alisema kuwa awamu ya kwanza ya mafunzo hayo yalishirikisha mikoa ya Kanda ya Pwani kama vile Dar es Salaam, Tanga, Mtwara,  Morogoro na Kilimanjaro, awamu ya pili katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Simiyu,  Geita, Mara, Kigoma na  Tabora na kuongeza kuwa awamu ya tatu inahusisha mikoa ya Iringa na Mbeya.
Alisema kuwa mafunzo haya ni endelevu na kusisitiza kuwa mikoa iliyobaki kama Katavi,  Rukwa, Njombe, Ruvuma, Dodoma, Arusha ambayo bado haijafikiwa itashirikishwa katika awamu ya nne.
Alieleza kuwa mpango huo wa miaka mitano ulioanza mwaka 2011 unatarajiwa kukamilika mwaka 2016.
Naye Kamishna Msaidizi wa Madini  Kanda ya Kusini Magharibi  Wilfred Machumu alisema kuwa mafunzo hayo yatatumika kama fursa ya maafisa mazingira kubadilishana uzoefu na changamoto katika usimamizi wa mazingira na hatimaye kupata mkakati wa pamoja wa kuboresha usimamizi wa mazingira.

No comments:

Post a Comment

TUPAMBANE BLOG