Blogger Widgets FURSA KWA VIJANA WOTE TUPAMBANE KWA KILA NJIA ILI MRADI TUWEZE KUEPUKA HUU UMASKINI TANZANI NA AMIN KILA ATAFUTAYE KWA NIA HUPATA MAANA ATA MAANDIKO HUSEMA PENYE NIA PANA NJIA

Saturday, November 1, 2014

Vijana jengeni ari ya kujiajiri



Vijana nchini wametakiwa kujenga ari ya kujiajiri huku wakijidhatiti kukabiliana na changamoto za ushindani katika soko la ajira.Wito huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein leo wakati alipokuwa akifungua kongamano la siku mbili kuhusu ajira kwa vijana linalofanyika katika Ukumbi wa Salama kwenye hoteli ya Bwawani mjini Unguja.
Vijana jengeni ari ya kujiajiri
Amewataka vijana kuukubali ukweli kuwa uwezo wa serikali wa kumpatia kila mhitimu ajira haupo hivyo vijana hawa budi kubadili mtazamo wao wa ajira kwa kuwa tayari kujiajiri na pamoja na kujiepusha na tabia ya kuchagua ajira pasi na sababu za msingi.
Alisema vijana hawana budi kuzingatia kaulimbiu ya kongamano hilo ambayo inawataka vijana kubadilika na kuchangamkia kila fursa ya ajira stahiki.Kuthibitisha kauli yake ufinyu wa nafasi za ajira serikalini alieleza takwimu zinaonesha kuwa tangu mwaka 2010 ilipoingia Serikali ya Awamu ya Saba imeweza kutoa nafasi za ajira 3,539 tu wakati ambapo kila mwaka maelfu ya wanafunzi wanahitimu elimu ya juu kutoka vyuo mbalimbali nchini na nje ya nchi.
Dk Shein aliwaeleza washirikiri wa kongamano hilo ambao wanatoka wilaya zote kumi za visiwa vya Unguja na Pemba pamoja kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuweka mazingira mazuri ambayo yatawezesha kutoa fursa zaidi za ajira kwa vijana zikiwa za kuajiriwa na kujiajiri.
Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuimarisha mazingira ya uwekezaji ambapo wawekezaji zaidi waweze kuanzisha miradi na biashara ambazo zitatoa ajira kwa vijana pamoja na Serikali kuanzisha mpango wa uwezeshaji kiuchumi wa wananchi wakiwemo vijana.Hata hivyo hatua hizo alieleza hazitakuwa na faida endapo vijana wenyewe hawatakuwa tayari kuzitumia ipasavyo fursa hizo kwa kuonesha umakini na uadilifu katika ajira wanazopota na pia kujipanga kuanzisha miradi itayaowawezesha kutumia fursa za mikopo zilizoanzishwa kwa ajili hiyo.
Alisisitiza kuwa itakuwa ni dosari kubwa kwa nchi kushindwa kuvutia wawekezaji kwa sababu tu vijana wake hawapendi kazi au hawana taaluma ya kutosha katika fani muhimu kuwezesha uwekezaji kustawi.Dk. Shein aliwataka vijana kuiangalia sekta ya kilimo ambayo Serikali imekuwa ikiwekeza sana kwa kutoa ruzuku ya asilimia 80 ya pembejeo kuwa ni sekta ambayo itawapatia ajira za haraka na serikali iko tayari kuwaunga mkono kwa wale wataoamua kujiingiza katika sekta hiyo.
Aliwatoa wasiwasi kuwa kamwe hawatalima kizamani kama ilivyokuwa kwa wazazi wao bali watapatiwa mbinu za kisasa pamoja na huduma nyingine kama matrekta na zana nyingine za kilimo.Aliwakumbusha vijana umuhimu wa kuutumia vyema ujana wao kwa kufanyakazi kwa bidii na kujiwekea akiba ya uzeeni kwa kuacha mambo yasio na msingi.
Katika hotuba yake hiyo iliyoamsha ari kwa vijana Rais wa Zanzibar alikubali ombi la vijana hao la Serikali kuongeza nafasi za elimu ya juu lakini akatahadharisha kuwa itafanya hivyo kwa fani na taaluma ambazo ni kipaumbele kwa nchi hivi.
Katika risala ya vijana hao iliyosomwa na kijana Lelya Mansoor Abdalla mbali ya kuiomba Serikali kuongeza fursa za elimu ya juu waliomba pia kufanyiwa marekebisho mitaala ya vyuo ili kuwawezesha wahitimu kuajiriwa na kujiajiri.Aliwakumbusha vijana kuwa sera na mipango inayoendelea kutekelezwa kuimarisha maendeleo na maisha yao ni kuendeleza fikra na malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Hivyo aliwataka vijana kukumbuka wajibu wao wa kuendeleza fikra na malengo ya Mapinduzi kwa kuhakikisha kuwa wanalinda amani na utulivu uliopo nchini ambao ndio msingi wa maendeleo yaliyopatikana hadi sasa.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Kaimu Waziri wa Kazi na Utumishi wa Umma Haji Omar Heri aliwahakikishia vijana kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itayafanyia kazi matokeo ya kongamano hilo ili kufikia malengo yanayotarajiwa.
Alibanisha kuwa Serikali imekichukua kwa uzito kilio cha Chama cha Waajiri Zanzibar-ZANEMA cha kutaka Serikali kuwandaa vijana wanaohitimu vyuoni wanaweza kuajirika na kumudu majukumu yao ipasavyo.Alisema kongamano hilo ni fursa adhimu kwa vijana na wadau wengine kulichambua kwa kina tatizo la ajira kwa vijana kwa kuangalia hali iliyokuwa, ilivyo sasa na kutoa muskabala wa siku zijazo.
Waziri Omar ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum alitumia fursa hiyo kuwashukuru wadau mbalimbali walifanikisha kongamano hilo likiwemo Shirika la Kazi Duniani- ILO. 
Akitoa maelezo kuhusu washiriki wa kongamano hilo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma Bi Fatma Gharib Bilal alisema kuwa miongoni mwa washiriki ni vijana walioajiriwa, waliojiajiri miongoni mwao wakiwemo waliopata mafanikio, walio nje ya ajira ambao wanatarajia kujiajiri, walio vyuoni pamoja na waajiri.

No comments:

Post a Comment

TUPAMBANE BLOG