Mbali na kuongoza kuwa chakula kikuu na kukidhi mahitaji ya mkoa huo, walaji wa mikoa mingine ya Tanzania kwa jumla sehemu ya mahitaji ya ndizi hutoka mkoa wa Kagera.
Hata hivyo, juhudi za mkoa huo kuendelea kuwa kitovu cha ndizi, zinakabiliwa na changamoto kadhaa baada ya kuibuka ugonjwa unaoshambulia migomba uitwao mnyauko bakteri au unyanjano.
Ingawa una jina lake la kisayansi, ugonjwa huo kwa wazalishaji wengi wa ndizi una jina lake maarufu, unaitwa Ukimwi wa migomba na unaonekana kuenea kwa kasi katika maeneo mbalimbali mkoani humo.
Wataalam wa magonjwa ya mimea wameanza kuamini kuwa kasi na madhara ya ugonjwa huo kwa migomba, utaweza kusababisha njaa iwapo hautadhibitiwa haraka.
Baada ya ugonjwa huo kusambaa mkoa mzima, wataalam wa kilimo wanachukua hatua za kukabiliana nao, wanafanya juhudi ya kuleta mbegu za kisasa za migomba ili kuzalisha mimea ya zao hilo ambayo ni tofauti na migomba ya asili.
Lakini wakati juhudi hiyo inachukuliwa wakulima wana wasiwasi, wana hofu kwamba mbegu za migomba ya kisasa zikichanganywa na za migomba ya asili, migomba ya asili haistawi vizuri kwa maelezo kuwa migomba ya kisasa inaharibu udongo.
Pamoja na kulalamikiwa, migomba ya kisasa bado inatajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuvumilia magonjwa mbalimbali yanayoshambulia zao hilo, isipokuwa ugonjwa wa unyanjano.
Hata hivyo wasiwasi huo haujazuia juhudi za wataalam kukabiliana na changamoto za kilimo cha zao hilo, baadhi ya wananchi wanaendelea kulima na kupanda migomba ya kisasa na ya asili lakini wanapunguza kasi ya kupanda ile ya asili.
Mwanahawa Khalid, mkazi wa kijiji cha Kashaka wilayani Missenyi, ni mmoja wa wakazi wa eneo hilo wanaofanikiwa kutegemea chakula cha ndizi zinazotokna na migomba ya kisasa.
Anasema anaendesha kilimo hicho kwa kushirikiana na mume wake Khalid Abibu na kuwa walianza kilimo cha migomba hiyo mwaka 2002 kwa kutumia mbegu kutoka kituo cha utafiti wa kilimo cha Maruku wilayani Bukoba.
“Wakati tunaanza kilimo cha migomba hii ya kisasa tulianza na shamba lenye ukubwa wa ekari tisa, lakini sasa tumekwishafikisha shamba lenye ukubwa wa ekari 11,” anasema Mwanahawa, mama mwenye waoto 11.
Anasema kuwa kutokana na kilimo hicho wana uwezo wa kuvuna mikungu ya ndizi kuanzia 150 hadi 400 kwa mwezi kutegemea na msimu na kuwa kila mkungu unauzwa kati ya shilingi 10,000 hadi 13,000.
“Wakati wa kiangazi kutokana na kuwepo kwa ndizi nyingi kawaida tunauza mkungu wa ndizi kwa shilingi 10,000 lakini katika misimu mingine yenye uhaba wa ndizi, tunauza mkungu mmoja kati ya shilingi 12,000 hadi 13,000,” anasema Mwanahawa.
Kutokana na uzalishaji huo, endapo wanafamilia hao wataweza kuzalisha na kuuza mikungu 400 kwa mwezi kama ilivyoelezwa, wataweza kujipatia Sh. Milioni 4 kwa mwezi, sawa na Sh. Milioni 40 kwa mwaka.
Anasema ndizi wanazovuna katika shamba lao husafirishwa na kuuzwa katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga, na kuwa wafanyabiashara wengine wakiwamo wa kununua mikungu michache, hufuata ndizi shambani.
Anasema, wakati wameanzisha kilimo hicho walikuwa wanatembelewa na wataalam wa kilimo kutoka wilaya ya Missenyi, lakini sasa hawafanyi hivyo tena.
Anasema hali hiyo imesababisha wakulima kufanya kazi ya kilimo kwa uzoefu bila kuwa na ushauri juu ya mbinu mpya zaidi za maendeleo ya kilimo hicho.
Akizungumzia mafanikio waliyoyapata kutokana na kilimo hicho, Mwanahawa anashukuru kwamba hawana shida ya kukosa chakula na pia pesa kidogo kwa mahitaji ya kila siku na kuwasaidia watoto kwenda shule.
Mwanahawa anasema kuwa, watoto wao wengine ambao walishindwa kuendelea na elimu ya juu wamewezeshwa kujitegemea baada ya kupewa msaada kutokana na mafanikio ya kilimo cha ndizi.
Anasema ili kuzuia ugonjwa wa unyanjano kuhamia katika mashamba jirani na kuingia katika shamba lake, wakulima wanaondoa ua dume mapema ili kuzuia wadudu kama nyuki kusambaza ugonjwa huo.
Anawashauri wananchi wenzake kujiunga na kilimo cha mazao kama njia ya kupata maisha bora, ikiwamo kujitosheleza kwa chakula na pia kuondokana na tatizo la ajira.
Mtafiti mkuu wa kituo cha utafiti Maruku, Leonard Mukandala anasema kuwa, utafiti wa kupata mbegu mbadala ambayo haishambuliwi na ugonjwa huo unaendelea, amewataka wananchi kuendelea kufuata ushauri wa kitaalam wanaopewa ili kupunguza maambukizi.
Mukandala anasema kuwa, pamoja na ushauri huo wananchi wanatakiwa kutumia mbegu za migomba isiyo na maambukizi kutoka katika vitalu 117 vilivyoko katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, ambavyo vilianzishwa ili kupambana na ugonjwa huo.
Anataja njia nyingine za kupambana na ugonjwa huo kuwa ni kusafisha vifaa kwa kutumia jiki au moto kila baada ya kuvitumia, kutoruhusu ua dume kukaa muda mrefu kwenye mgomba na kutoazima vifaa vinavyotumika katika shamba kwa mtu mwingine.
Kuhusu malalamiko ya wakulima ya migomba ya kisasa kuharibu udongo na kusababisha migomba ya kisasa kutostawi, anakana na kudai kuwa migomba hiyo haiharibu udongo bali ina nguvu sana ya kufyonza chakula kuliko ya asili hivyo wakati wa kulima wakulima hawatakiwi kuichanganya katika shamba moja.
“ Migomba ya kisasa ina nguvu sana kuliko ya asili, ili migomba ya asili isiathirike lazima mkulima atenge shamba lake na apande mazao hayo kwa kuyatenganisha, ya asili ipandwe peke yake na ya kisasa ipandwe peke yake” anasema Mukandala.
Anasema kuwa pamoja na kutenganisha migomba hiyo pia wananchi wanapaswa kuweka mbolea na kutunza mashamba yao vizuri ili waweze kupata mavuno mengi.
Anasema siyo kweli kuwa migomba ya kisasa haishambuliwi na ugonjwa huo wa unyanjano na kuwa migomba yote inashambuliwa tena kwa kiwango sawa ila kinachotakiwa ni kulitunza shamba vizuri na kufuata taratibu za kitaalam.
“Uzuri wa migomba ya kisasa (fia) inavumilia magonjwa mengine lakini siyo ugonjwa wa unyanjano, ugonjwa huu unaenezwa na vimelea aina ya bakteria hivyo unashambulia migomba ya aina yote, mgomba ukipatwa na ugonjwa huu lazima ufe” anasema.
Mkuu wa mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe, anasema kuwa ugonjwa wa unyanjano ni janga maana zao linaloshambuliwa ni tegemezi kwa wakazi wa mkoa huo kwa chakula na biashara.
“Asilimia 50 ya ndizi zinazouzwa hapa Tanzania zinazalishwa Kagera, hivyo linavyoendelea kushambuliwa na ugonjwa linaathiri upatikanaji wa chakula na kipato maana sasa pia ni zao la biashara” anasema Kanali Massawe.
Anasema ugonjwa huo kushambulia migomba sio kwa mara ya kwanza maana mwaka 1952 wakati wa ukoloni ulizuka na kudhibitiwa haraka na kutoweka mwaka 1956 kutokana na sheria kali za kikoloni.
Anasema, mwaka 2006 ugonjwa huo ulirudi tena na kuanza kuonekana katika wilaya ya Muleba na sasa umeenea mkoa mzima na mikoa mingine jirani ikiwamo wilaya ya Tarime mkoani Mara, Ukerewe mkoani Mwanza na Kibondo mkoani Kigoma.
Akizungumzia hali ya kiwango cha maambukizi anasema wilaya ya Kyerwa inaongoza kwa kuwa na familia zilizoathirika asilimia 75, ikifuatiwa na wilaya ya Karagwe yenye familia zilizoathirika asilimia 70.
Anasema kuwa wilaya ya Bukoba familia zilizoathirika ni asilimia 65, wilaya ya Muleba asilimia 60, wilaya ya Missenyi asilimia 35, wilaya ya Ngara asilimia 30 na wilaya ya Biharamulo asilimia 25.
Anasema, kutokana na kiwango cha maambukizi kuonekana kuwa juu serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa kilimo, wanaendelea kuelimisha wananchi namna ugonjwa huo unavyoenea na jinsi ya kuudhibiti.
“Tumeunda vikosi kazi ambavyo vinatembea mkoa mzima kuelimisha jamii, lakini pia tumetoa mafunzo kwa maafisa ugani kuhusu namna bora za kuudhibiti ugonjwa huo na hatua za kuchukua kwa wale ambao tayari mashamba yao yana maambukizi,” anasema.
Anasema ili kuudhibiti ugonjwa wa unyanjano kwa haraka, katika mwaka wa fedha 2012/2013 serikali ya mkoa ilitoa agizo kila halmashauri kutengeneza sheria ndogo ili wananchi watakaobainika kuueneza kwa uzembe wahukumiwe kifungo cha miezi sita, ili wengine wajifunze.
“Nimeagiza viongozi wote kuanzia Januari mwakani, viongozi wote kuanzia ngazi za vitongoji lazima washiriki kuutokomeza, eneo utakapoonekana ugonjwa huo, mkulima lazima afikishwe mahakamani na mtendaji wa eneo husika kazi yake itakuwa hatarini,” anasema kanali Massawe.
Anasema halmashauri zote mkoani Kagera zinatakiwa kutenga fedha katika bajeti ili zisaidie katika mapambano na kuwa serikali imedhamiria mwaka 2014 iwe ndiyo mwisho wa ugonjwa huo.
Kutokana na kutokuwepo kwa dawa ya kudhibiti ugonjwa huo, maelekezo ya kitaalam yanawataka wananchi kung’oa migomba yote iliyoathirika kuichoma moto na kisha kuchimba shimo na kuifukia ili isiambukize migomba mingine.
Wakati mkuu huyo wa mkoa akidai ugonjwa huo ni tishio kwa uchumi wa wananchi wa mkoa wa Kagera, pato la mwananchi katika mkoa huo kwa sasa linakadiriwa kuwa ni shilingi 800,000 kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment