KILIMO
cha zao la mahindi kimeendelea kuonekana kama ni njia mbadala ya
kumkomboa mwananchi wa kawaida na hasa kwa mikoa ya nyanda za juu
Kusini, lakini pia ushiriki wa karibu wa Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya
Chakula (National Food Reserve Agency (NFRA), kumechangia kuongeza
hamasa katika sekta hiyo muhimu kwa maisha na maendeleo ya wananchi na
hasa wa vijijini.
Nilitembelea
mikoa hiyo na nikaangazia kilimo hicho kwa mikoa ya Njombe, Iringa na
Mbeya, inayofahamika kama kanda ya Makambako ya NFRA, inayohuduma wilaya
za Njombe, Ludewa, Makete, Wanging’ombe, mkoani Njombe na wilaya za
Mbarali, Mbeya, Chunya, Ileje na Mbozi, katika mkoa wa Mbeya.
Kwa
kuanzia nilikutana na Meneja wa Kanda hiyo, (Makambako Zonal Manager)
Abdillah Nyangassa, ambaye pamoja na mambo mengine alitoa ufafanuzi
kuhusu hali ya soko la mwaka 2013/2014 na mafanikio yake kwa wakulima.
Licha
ya kuwepo kwa changamoto za hapa na pale, Nyangassa, anasema NFRA kama
chombo cha serikali, hakifanyi kazi zake kisiasa na kimeweza kufikia
malengo yake kulingana na bajeti ya fedha zinazotengwa na serikali
kwenye bajeti.
Kilimo
cha mazao ya chakula na biashara ni moja kati ya nguzo muhimu kwa
maisha ya wananchi wa mikoa inayohudumiwa na kanda ya Makambako ni
sejemu ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, awali ilipewa jina la The Big
Four, likimaanisha mikoa yenye nguvu za uzalishaji mkubwa kwa mazao ya
chakula.
Kanda
ya Makambako yenye vituo vya Vwawa wilaya ya Mbozi, Isongole wilaya ya
Ileje mkoa wa Mbeya, ambako uzalishaji wa mahindi umekuwa mkubwa na
unaoongezeka kila siku hivyo kuwapo kwa ziada ya chakula kwa familia
hununuliwa na serikali kwa ajili ya akiba ya Taifa kupitia NFRA.
Aidha,
NFRA kanda ya Makambako, kwa mujibu wa Nyangassa, hutumia vituo vya
Igwachanya katika wilaya ya Wanging’ombe, Shauri Moyo, Mawengi,
Mlangali, Ludewa Kijijini, wilayani Ludewa, lakini ni vituo maalum
vinavyotumika kwa ajili ya ununuzi na uhifadhi kwa muda tu.
Pia
hukitumia kwa ajili ya manunuzi na uhifadhi mahindi hayo Kituo kikuu
cha Kanda hiyo kilichopo katika mji wa Makambako wilayani Njombe, mkoani
Njombe, ambako pia kuna maghala makubwa ya kuhifadhia chakula, lakini
pia utunzaji baada ya kupulizia dawa hufanyika kwa ustadi mkubwa, ili
kuondoa wadudu waharibifu wa mazao.
Hata
hivyo, Nyangassa, anasema bayana kuwa wakulima wanaitegemea kwa kiasi
kikubwa NFRA katika kufikia malengo ya kilimo, kwa maana ya kuongeza
tija na uzalishaji pamoja na mavuno, huku akisisitiza bajeti kwa ajili
ya wakala hiyo inafanywa kulingana na uwezo wa kuhifadhi chakula.
Anasema
NFRA imefanikiwa kununua ununuzi katika vituo vilivyopo katika wilaya
ya Ludewa kiasi cha zaidi ya tani 2,500 za mahindi ya wakulima, SACCOS,
AMCOS na vikundi maalum na ambavyo tayari vimetambuliwa na NFRA vya
wafanyabiashara, ambapo kulingana na takwimu za wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika za mwaka 2010/2011, zaidi ya watu milioni 8.6
wanakitegemea kilimo cha zao la mahindi katika mikoa inayohudumiwa na
kanda ya Makambako.
Nyangassa
anasema ya kwamba msimu wa ununuzi wa mwaka huu, NFRA imetumia SACCOS
na AMCOS, kwa nia ya kushiriki kufufua ushirika na kuwa tayari wilaya za
Ileje, Mbozi, Wanging’ombe, Ludewa na Njombe, zimeanzisha mwendo.
“Ni
safari ya kuelekea kuviwesha vikundi vya wakulima, na hii ndio lengo
kuu la kuongezesha ushawishi kwa wakulima kujiunga katika vikundi vya
ushirika au vikundi jamii, kwani wanaweza kupitia njia hiyo hata misaada
ya serikali ya mafunzo ya kilimo bora na hata kuwezeshwa,” alisema
Nyangassa.
Hata
hivyo, Nyangassa, anasema ya kwamba, mpaka zoezi la ununuzi
linasitishwa, bado kuna baadhi ya wakulima wenye mahindi majukumbani,
akisema hatua hiyo ilitokana na wengi kudhani kuwa bei ya Sh. 500 kwa
kilo moja ya mahindi iliyokuwa ikitumika baada ya kufunguliwa kwa soko,
inaweza kuongezeka.
Kulingana
na Nyangassa, katika kituo cha ununuzi cha NFRA cha Mawengi
kinachounganisha vijiji vya Mbwila, Kiwe, Madunda, Lupande na Mawengi
yenyewe, kuna malalamiko kwamba kuna kiasi kikubwa cha mahindi ya ziada
kilichobaki kwa wananchi, lakini akasema hatua hiyo inalenga kuweka
tahadhari kwa jamii.
“Unajua
wakulima na wananchi wakiliona soko zuri kama lilivyo la NFRA,
wangehitaji kuendelea kuuza mazao yao, lakini kitu kikubwa na cha muhimu
ni kwamba NFRA inanunua ziada ya chakula hicho na wala sio mavuno yote
ya msimu,” anasema Nyangassa.
Anasema
ili kutambua hali ya mavuno, NFRA huwatumia watendaji na wenyeviti wa
vijiji na vitongoji katika kupata taarifa sahihi, ili kuondokana na
dhana ya kufunguliwa kwa vituo kisiasa hatua ambayo baada ya muda mfupi
hufuatiwa na malalamiko ya upungufu mkubwa wa chakula na njaa.
“Tunafanya
hivyo huko Mlangali, kwa kuwatumia viongozi kama Paschal Mayumbwa,
mwenyekiti wa kitongoji cha Mlangali Ndani, Renato Kahako Willa,
mwenyekiti wa kijiji cha Mawengi, Adriano Mwinuka, wa kijiji cha Shauri
Moyo, na wengine ili kujua hali halisi ya mavuno,” anasema Nyangassa.
Alhaji
Nyangassa, alisema kwamba baadhi ya vijiji wilayani humo vimekuwa na
kasi ya uzalishaji wa mahindi mwaka hadi mwaka, ikiwa ni pamoja na
Shauri Moyo, Ludewa, Mawengi na Mlangali, lakini hiyo inatokana na
uhakika wa soko la NFRA.
“Kwa
hakika wakulima wengi wanafanya hivyo kwa nia ya kulikimbia soko la
walanguzi ambao hivi sasa wako tayari na wanazunguka katika maeneo ya
vijijini wakitaka kununua mahindi hayo kwa bei ndogo, ambayo kwa kweli
haina msaada na manufaa kwa mkulima,” anasema Nyangassa.
Mkuu
wa wilaya ya Wanging’ombe, DC Esterina Kilasi, aliliambia gazeti hili
kwamba kazi nzuri inayofanywa na NFRA ndiyo inayochochea kasi ya
wananchi kuongeza maeneo ya kilimo cha mahindi kwenye wilaya yake.
“Wakulima
wetu wameanza kuona fulsa muhimu za kushiriki kilimo cha mahindi na
hili ni kutokana na kuwapo kwa uhakika wa soko la mahindi la NFRA kanda
ya Makambako, binafsi kama sehemu ya serikali nimefarijika, na
ninawapongeza watendaji hao kwa kazi nzuri na ya kupigiwa mfano” alisema
DC Kilasi.
Mkuu
huyo wa wilaya, alisema mbali na kufarijika kwa uhakika wa soko hilo la
serikali, lakini pia ukaribu na utaratibu mzuri wa NFRA kufungua masoko
katika vijiji vya Igwachanga na Igalala ndani ya wilaya yake.
“Wakulima
wengi sasa wameanza kuona umuhimu wa kuwepo kwa serikali na hasa baada
ya kufunguliwa kwa masoko kwenye vijiji vyao, badala ya hapo awali
ambapo walilazimika kulifuata kwa umbali mrefu soko la NFRA au la
wanunuzi wengine,” alisema DC Kilasi na kuongeza kuwa hatua hiyo
imepunguza adha ya walanguzi kuwalaghai wakulima.
Kwa
upande wake, Mkuu wa wilaya ya Ludewa, DC Juma Madaha, alisema kuwa
NFRA imeisadia serikali kupunguza malalamiko ya wakulima hasa wanapokosa
soko la uhakika la mazao yao, licha ya kuwapo kwa hamasa kubwa.
“Tunatumia
muda mwingi kupita vijijini kwa ajili ya kuhamasisha wakulima na hasa
vijana kuendelea kushiriki katika kilimo, hivyo ni matarajio yetu kuwapo
kwa uhakika wa soko la mazao hayo,” alisema DC Madaha.
Mkuu
huyo wa wilaya alisema fulsa pekee ya wazi kwa mkulima wilayani humo ni
kuona vituo na masoko ya NFRA yanayozunguka kwenye maeneo ya vijijini,
(mobile buying centers), na kuongeza kwamba mfumo huo umewapunguzia
usumbufu wananchi.
Baadhi
ya wakulima wa mahindi akiwamo Agnes Mkinga, wa kijiji cha Mawengi,
wilayani Ludewa, alisema na kuishukuru NFRA kanda ya Makambako kuchukua
maamuzi ya kufungua vituo vya ununuzi kwenye maeneo ya vijijini ambapo
pia ilitangaza bei ya msimu kuwa Sh. 520.
Mkinga
alisema hatua hiyo ya kutangaza bei nzuri iliwafariji wakulima kwa
kiasi kikubwa, lakini wengi walikuwa hawajamaliza kuvuna mahindi yao,
hivyo mpaka vituo vinafungwa kutokana na kufikiwa kwa malengo ya ununuzi
bado kulikuwa na kiasi kikubwa cha mahindi.
“NFRA
imefanya mambo makubwa kwa wakulima wa mahindi, na kwa hakika mahindi
yakiwekewa mkazo, yanaweza uhamasishaji kama ambavyo Rais Jakaya
Kikwete, alivyosema wakati alipokuja kwenye ziara na uzinduzi wa mkoa
mpya wa Njombe, kwamba mazingira yakiboreshwa kilimo cha mahindi
kitakuwa mkombozi wa maisha ya wananchi wengi zaidi lakini pia akitaka
kuondokana na uvivu” alisema Mkinga.
Wakulima
wengine pamoja na kuishukuru Serikali kwa majukumu ya uhakika
yanayofanywa na NFRA, lakini walishauri wakala hiyo kuongezewa majukumu
ili kulihudumia zao la mahindi kama kweli nia ni kuona tija.
“Lakini
pamoja na mambo mazuri na hasa kwenye kununua mahindi, sasa ni vyema
NFRA ikapewa na serikali majukumu ya kusambaza mbolea kwa wakulima na
hasa kwenye maeneo yenye vituo vya ununuzi,” alisema Michael Komba,
mkazi wa Ludewa.
“Kuja
na kununua mahindi ya wakulima kwa ajili ya hifadhi ya Taifa bila
kuiwezesha NFRA kujenga mtandao usiokuwa na shaka ya wapi kumepatikana
mavuno mengi katika msimu sio matumizi bora ya rasilimali na yenye
tija,” alisema mkulima Hilda Mgaya.
Mkulima
huyo alisema kukosekana kwa pembejeo za uhakika na hasa kutoka katika
ofisi za serikali, kumechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa wauzaji
wa mbolea feki inayoangamiza ardhi na kudumaza mavuno ya mazao.
“Lakini
pia kukosekana kwa soko la muda mrefu kwa maeneo ya vijiji kamwe
hakukidhi haja ya kilimo, kwani mwaka jana mahindi mengi yalikosa ubora
na yaliozoea kwenye nyumba za wananchi, hivyo pamoja na serikali
kutakiwa kuongeza fedha, lakini pia kuipa NFRA jukumu la kusimamia
mbolea vijijini,” alisema Hilda Mgaya.
Mwenyekiti
wa Muungano wa vikundi vya wakulima wadogo wa mahindi katika wilaya za
Iringa Vijijini na Kilolo, Yohanes Mhanga, alisema kwamba japo soko la
NFRA ni la uhakika kwa mkulima, lakini bado lipo mbali na maeneo yao ya
kilimo.
Mhanga
alisema ya kwamba soko hilo la NFRA limesaidia kuwaongezea ujasiri
wakulima wengi wa vijijini waliokuwa wakihujumiwa na baadhi ya
wafanyabiashara na walanguzi, kukabiliana na hali hiyo kwa kuikimbilia
wakala hiyo.
Mhanga
alisema ni vyema serikali ikakubali kuongeza fedha ili kuipatia nguvu
na uwezo NFRA, kufanya utafiti wa hali ya chakula nchini, badala ya
kutumia taarifa nyingi za mezani za maafisa kilimo wa wilaya.
“Maafisa
wengi hawaendi vijijini, wanafanya makadirio ya kimazoea, lakini
wananchi wengi wanalima na wanavuna mahindi mengi, lakini kwa vile wao
wanaendelea na majukumu yao ya kimazoea, NFRA bado haijaliona eneo letu
kama lenye uzalishaji mkubwa wa mahindi,” alisema Mhanga.
Mmoja
wa wakulima wakubwa wilayani Mbozi, Jeremiah Isso, aliliambia gazeti
hili katika mahojiano maalum kwamba NFRA tayari imesaidia kwa kiasi
kikubwa kuwajengea ujasiri wa kiuchumi na kuwakomboa wakulima wengi.
“Leo
mkulima wa mahindi anatambiana na mkulima wa pamba, kahawa na hata
tumbaku, na hii ni kutokana na uhakika wa soko la NFRA, hivyo naiomba
serikali ifanye mapinduzi makubwa ya kibajeti kwa kuiangalia NFRA ambayo
sasa inahudumia wananchi vijijini,” alisema Isso.
Mratatibu
wa shughuli za kilimo cha mahindi katika wilaya ya Ileje, Deogratius
Mtewele, alisema kilimo cha mahindi kimeendelea kuwa mkombozi kwa
wananchi wengi, lakini pia akishukiuru NFRA na wizara ya kilimo kwa
kuwathamini wananchi.
Mtewele
alisema kwa mara ya kwanza NFRA mwaka huu imetoa bei nzuri na ambayo
imewafariji watu wengi, lakini pia matumizi ya Soko la Kimataifa la
Isongole, kama kituo cha ununuzi.
“Kwa
kweli tumefarijika na NFRA, lakini pia matumizi ya soko hili la
Isongole, lililojengwa kwa nguvu za wananchi wa nchi mbili za Malawi na
Tanzania, nalo limeendelea kuwa kivutuo muhimu cha ununuzi wa mahindi ya
wakulima wa wilaya hiyo na maeneo ya jirani,” alisema Mtewele.
No comments:
Post a Comment