Wakati haya yakitokea serikali imetakiwa kutafuta suluhisho la kudumu ili kuondoa kabisa matatizo ya mara kwa mara yanayotokea wakati wa mvua za masika, na kusababisha marufiko hususani katika mkoa wa Dar es Salaam.
Katika Makala haya Tupambane itaangazia nani anawajibika au anahusika wakati maafa yanapotokea nchini Tanzania na je tunasaidianaje kupunguza madhara ya maafa yanayotokea nchini yakiwemo maeneo yaliyozoeleka kuwa yanaweza kuathiriwa na maafa yanapotokea.
Ukosefu wa elimu
Aidha, katika moja ya mahojiano ya Tupambane na wakazi wa maeneo mbalimbali nchini wanabainisha kuwa maruriko yanayoendelea kutokea nchini yanakuwa tatizo kubwa kwa jamii na kusababisha umaskini kwa kuifanya serikali kuingia gharama kubwa kwa kuhifadhi wakazi wanaokumbwa na janga la mafuriko.
Wamebainisha kuwa moja ya shughuli zinazotakiwa kufanywa na serikali ili kutatua tatizo hili ni kutembelea maeneo korofi yanayokumbwa na matatizo ya mafuriko mara kwa mara na kuendesha warsha kwa wanafunzi wa shule za Sekondari ili kuwahamasisha kusomea mafumo ya Sayansi kwa manufaa ya kizazi kijacho.
Mbali na tatizo hili nimeelewa kuwa pia serikali inatakiwa kuwaandaa wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi, ili kuepuka hasara zinazojitokeza katika misimu ya kilimo ikiwemo ya mavuno kwa kuwa wengi wao wanategemea mvua ambazo hazinyeshi kwa wakati hivyo kusababisha baadhi ya maeneo kukumbwa na janga la njaa.
Mtaalamu wa Mazingira na Kilimo kutoka Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa wadudu waharibifu wa Ikolojia nchini Kenya, Dkt. Birigita Nyambo, anasema matokeo ya utafiti wa athari za mabadiliko haya uliofanywa mkoani Kilimanjaro yameonyesha kuwa wakulima wengi nchini Tanzania hawaandaliwi ipasavyo ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kuwa wengi huendelea kulima kilimo cha mazoea cha kutegemea mvua pasipokuw ana mbinu mbadala za kuzalisha chakula.
Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, Kanda za Juu Kaskazini Mashariki, Joharia Mshana, anaeleza kuwa wakulima mkoani Kilinjaro hawazingatii utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) lakini pia anawataka wakulima hawa na maeneo mengine kuacha kutegemea utabiri wa asili ili kuepuka hasara ambazo wamekuwa wakipata msimu wa kilimo.
Takwimu zinaonyesha kwamba vifo 851 tangu mwaka 2011/2012 vilitokana na madhara ya mafuriko, na watu takribani milioni 1.7wameathiriwa na majanga ya mvua na nyumba takribani elfu 11 na mifugo 7,000 zilipotea na serikali ilitumia bilioni 20 kupambana na majanga haya. Kwa ujumla takwimu hizi zinatuonyesha kwamba hatujaamua kupambana na hili janga na hakuna ushirikiano wa kutosha kati ya serikali na Mashirika yasiyo ya kiserikali (NG’Os) na katika hili ninaomba ushirikiano uboreshwe na kudumishwa kati ya serikali na Ngo’s ili kukabiliana na hali hii pamoja, wananchi na wadau wote wanaohusika.
Christina Msanya, ni mwananchi wa kawaida kutoka mkoa wa Morogoro anasema njia bora ya mawasiliano ya kuwafikia wananchi pindi maafa yanapotarajiwa kutokea kwa upesi, anasema TMA wakijizatiti kutoa taarifa mapema zaidi na kuainisha maeneo yatakayoathiriwa na hali husika itasaidia kuepuka kuwachanganya kama njia bora ya kuepuka majanga.
“Wanasema leo mvua itanyesha Morogoro ukakuta mvua inanyesha upande wa Ifakara au maeneo mengine lakini hapa mjini hakuna mvua, tunaomba wawe makini kwa kuangalia maeneo”.
Kuharibika kwa miundombinu ya barabara
Anasema suala la usafiri limekuwa kero pindi maafa yanapotokea na kwamba jambo linalotakiwa kufanyika katika kipindi hicho ni serikali kuwa tayari kwa kukabiliana na hali yeyote inayoweza kutokea.
Gerald Haule, ni mkazi wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, anasema kwa kuwa serikali inakamati za kushughulikia maafa yanapotokea, kamati husika hususani kwa upande wa mkoa na wilaya janga limetokea kamati inatakiwa kuratibu shughuli zote na sio upande wa usafiri tu bali hata masuala ya kiafya ili kuhakikisha wale wanaoenda kutoa msaada maeneo yaliyoathiriwa yanafikiwa kwa urahisi zaidi (magari yapite kwa njia mbadala) hata kama kuna shughuli nyingine zilizokuwa zimepangwa magari hayo ynatakiwa kuchukua hatua ya kushughulikia suala hili.
Utata wa taarifa za TMA
Kwa sasa TMA imeithibitishia tupambane kwamba taarifa zake zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa, wengi watakuwa mashuhuda jinsi hali ya hewa ilivyotokea mwaka huu, Kitengo cha Utabiri wa Hali ya Hewa kilitoa tahadhari katika maeneo yote kama mtakavyokumbuka mafuriko yaliyotokea jijini Dar es Salaam na Kilosa mkoani Morogoro.
Tahadhari ilikuwa imetolewa mapema kabisa kwamba katika maeneo hayo hali ya mvua inatarajiwa kuongezeka na waliokuwa wanaishi katika maeneo hayo walitakiwa kuchukua tahadhari (madhara yalitokea kwa baadhi ya wananchi walioacha kuchukua tahadhari) na kwasasa hivi hali ya utoaji taarifa ya tahadhari katika hali ya hewa imeboreshwa kwa kiwango kikubwa.
Mwanzoni TMA ilikuwa haiainishi maeneo wanayotarajia kuwa yataathiriwa na mvua kiwilaya bali walikuwa wanataja kuwa kanda flani inatarajiwa mvua itanyesha kwa kiwango flani lakini kwa sasa wanataja kama ni mkowa wa Ruvuma, wanataja wilaya zake ambazo zinaweza kuathiriwa na mafuriko.
Utoaji wa misaada
Linapokuja suala la maafa ndipo serikali husisitiza kwa wakati ule kuwa wananchi mzingatie taarifa za wataalamu (TMA) na wakati suala hili linatakiwa kuzungumziwa kila mara ili wananchi waelewe, japo kuwa taarifa za TMA mara kadhaa zinadaiwa kuwa haziwafikii wahusika kwa wakati.
Debora John, mkazi wa Vingunguti Dar es Salaam, anasema serikali itoe elimu ambayo itaanzia shule za msingi na viongozi wa serikali za mtaa ambao wanaishi na wananchi ili wawafundishe jinsi ya kuepuka maafa yanayoweza kutolewa.
Mfumo wa awali wa tahadhari
Msimamizi wa Huduma za Hali ya Hewa kwa Jamii kutoka TMA, Hellen Msemwa, anasema mfumo huu wa tahadhari wa awali wa majanga yanayosababishwa na hali mbalimbali ya hewa inategemea na aina ya janga na kwamba mfumo huu unahusisha wadau mbalimbali na kwamba kunatakiwa kuwe na kituo cha kutoa tahadhari (warning center), Mamlaka za kuratibu maafa katika ngazi mbalimbali ikiwemo Taifa, mkoa, wilaya, na katika ngazi ya vijiji na kuwepo na wadau. Pia njia mbalimbali za mawasiliano (vyombo vya habari, vyombo vinavyotoa elimu kwa jamii, vyombo vinavyolinda usalama na mengineyo).
Anasema katika mfumo huu pia kuna kushirikisha wataalamu wa Kitaifa na Kimataifa katika kutoa huduma zinazolenga kupunguza madhara ya majanga husika na vilevile mfumo huu unahusisha jamii husika. Anaeleza kuwa TMA inaingia katika mfumo huu kama Kituo cha kutoa tahadhari ya majanga, au hatari zinazosababishwa na hali ya hewa kwa kuwa TMA inaangalia nini kinaweza kutokea kutokana na hali tarajiwa ambayo pia inatoa taarifa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kitengo cha maafa) na kisha kwenda kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na hali hii inatokana na daraja la tahadhari husika.
Ruhanda Oswadi, ni mtaalamu wa Udhibiti wa Majanga na Maafa katika mazingira kutoka Asasi ya Diprota, ambaye anabainisha kuwa mifumo ya tahadhari imegawanyika katika sehemu kuu tatu (Mfumo wa tahadhari kabla ya maafa kutokea, wakati yametokea na baada ya maafa kutokea).
Anasema mifumo ya kabla ya maafa kutokea inamsaidia mwananchi wa kawaida aweze kuepukana na athari zinazotokana na maafa (mafuriko au moto). Anasema hapa nchini kwetu Tanzania mifumo ya kutoa taarifa kabla ya maafa kutokea ni hafifu na utekelezaji wake hauifikii jamii moja kwa moja.
“Mfano mitandao ya simu ambayo ingeweza kutusaidia kutoa taarifa ya mapema kabisa kwa kila mtu mwenye simu wakati maafa yametokea pasipokuangalia kwenye Televisheni au kusikiliza Radio ingesaidia kwasababu tunapozungumzia tahadhari lazima tuangalie sheria ambayo yenyewe itasaidia wananchi kutambua tahadhari kabla ya maafa”.
TMA kwa sasa inapotoa tahadhari wasema wanafuatilia hali hiyo hadi itakapoisha, na wanavyowashauri wananchi kwamba wafuatilie taarifa zao, ni vyema zikafuatwa ili zisipuuzwe.
Wananchi wanatakiwa kuelewa kuwa utaratibu wa TMA kuwapa taarifa kupitia njia ya simu imeanza kwa baadhi ya maeneo ikiwemo katika Wilaya za Loliondo mkoani Arusha, Sengerema na pia katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Mwanza (kwa maeneo yanayopataka na Ziwa).
Nini kifanyike pindi maafa yanapotokea?
Mfano sheria inayohusu usafirishaji wa reli, inatoa mwongozo kuwa baiskeli ikigongwa na treni kwenye reli inamana baiskeli imegonga treni vivyo hivyo huku kwenye maafa sheria inatakiwa iseme kwamba atakayepewa tahadhari labda ya kutoka sehemu lenye hatari kwamba aende sehemu nyingine (salama) akikaidi mara tatu huyu mtu anatakiwa kupewa adhabu kwa kukiuka agizo la serikali.
Erick Buguzi, ni mwananchi wa kawaida kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro, anasema kwa mtazamo wake mwananchi awe mtu wa kwanza kuhusika kwa msaada wa serikali kutokana na kwamba ndiye anayeathirika moja kwa moja kwa kuwa akipewa elimu anaweza kukabiliana na hali hiyo.
“Serikali ichore ramani ili kuainisha maeneo yanayotazamiwa kupatwa na majanga (hili limeshaanza kufanyiwa kazi kwa kuainisha wilaya zinazoweza kuathiriwa) inatakiwa iseme kuanzia eneo hili hadi eneo flani kunaweza kuathiriwa na hali ya marufiko, elimu itolewe kwa kina, wananchi wakielimishwa watachukua hatua haraka katika kudhibiti matokeo ya majanga”.
Ninaamini kwamba serikali ni mdau mkubwa sana katika kudhibiti majanga haya sio lazima watu tuingie kwenye maafa, hii yote itasababisha kufanyika kwa maandalizi kabla ya janga kutokea na wahusika wajaribu kupata takwimu zilizosahihi ili ziende kwa haraka na kwa usahihi, pia wananchi na wadau wakuu wanaotakiwa kushirikishwa wapewe taarifa kwamaana serikali pamoja na kwamba ndiye mdau mkuu lakini pia taasisi nyingine zinatakiwa kushiriki katika kunasua majanga yanayotokea katika jamii.
No comments:
Post a Comment